Nasa waambiwa hakuna serikali ya mpito

Muktasari:

  • Mshauri mkuu wa sheria wa serikali alisema Rais Uhuru Kenyatta atakuwa na mamlaka yake yote aliyopewa kikatiba hadi hapo atakapoapishwa mkuu mpya wa nchi

Nairobi, Kenya. Mwanasheria Mkuu Githu Muigai ametupilia mbali uvumi ulioenea kuhusu mgogoro wa kikatiba katika kipindi hiki nchi inajiandaa kwa uchaguzi wa marudio wa kura ya rais.

Muigai, akizungumza jana kuhusu madai ya wanasheria wa kambi ya upinzani ya National Super Alliance (Nasa) yaliyotolewa hivi karibuni kwamba serikali ya muda au ya mpito itaundwa ikiwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (IEBC) itashindwa kusimamia uchaguzi, alisema wamepotoshwa.

Akizungumza ofisini kwake, mshauri huyo mkuu wa sheria wa serikali alisema Rais Uhuru Kenyatta atakuwa na mamlaka yake yote aliyopewa kikatiba hadi hapo atakapoapishwa mkuu mpya wan chi.

Mamlaka hayo alisema ni pamoja na kuwa Amiri Jeshi wa majeshi yote.

Wanasheria wa Nasa, wakiongozwa na James Orengo wameelezea kwamba mamlaka anayofurahia Rais Kenyatta ni ya “rais wa muda” kama ilivyoelekezwa na Ibara ya 134 ya Katiba.

Ibara hiyo inazungumzia kipindi kati ya siku ya uchaguzi na siku ambayo rais mteule anaapishwa kuwa rais kamili.

Muigai amesema hata hivyo, uhalali wa Rais Kenyatta hauwezi kuhojiwa.