Nasa washindwa kesi mbili mfululizo

Nairobi, Kenya. Idara ya mahakama nchini Kenya imesafishiwa njia ya kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Agosti 8 baada ya kutupilia mbali kesi mbili zilizohusu Muungano wa Upinzani (nasa).

Jana Mahakama ya Rufaa ilibatilisha uamuzi wa Mahakama Kuu wa kuzuia zabuni ya Sh2.5 bilioni iliyopewa Kampuni ya Al Ghurair kutoka Dubai kuchapisha makaratasi ya kura za urais. Mahakama Kuu iliruhusu kampuni hiyo iendelee kuchapa makaratasi ya kura za ugavana, ubunge na wanawake lakini si za urais.

Lakini ikipitia rufaa iliyowasilishwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Mahakama ya Rufaa ilisema hitaji la umma kushirikishwa katika utolewaji zabuni halikuwa na msingi.

Leo, Nasa wamepoteza kesi nyingine dhidi ya IEBC. Muungano huo unaoongozwa na mgombea wa urais, Raila Odinga ulipoteza ombi la kuitaka Mahakama Kuu iishurutishe tume kuahirisha uchaguzi ikiwa mfumo wa kielektroniki wa kupiga kura utakwama.

Katika ombi hilo, Nasa ilidai IEBC imeshindwa kuweka mfumo mahsusi kama inavyohitajika kisheria.

Lakini jopo la majaji watatu, Kanyi Kimondo, Hedwig Ong'udi na Alfred Mabeya wametupa kesi yao wakisema IEBC imeweka mikakati ya kukabiliana na tatizo la kufeli kwa mfumo huo wa upigaji kura.