Nassari agawa CD za madiwani waliojiuzulu kuanika ukweli

Muktasari:

  • Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari amemnadi mgombea udiwani wa Kata ya Ambureni, Dominick Mollel kwa kugawa CD anazodai zinaonyesha namna baadhi ya madiwani wa chama hicho wilayani Arumeru walivyoshawishiwa kupokea rushwa.

Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari amemnadi mgombea udiwani wa Kata ya Ambureni, Dominick Mollel kwa kugawa CD anazodai zinaonyesha namna baadhi ya madiwani wa chama hicho wilayani Arumeru walivyoshawishiwa kupokea rushwa.

Nassari aliyekuwa ameambatana na mbunge wa Bunda, Esther Bulaya aligawa zaidi ya nakala 500 katika mkutano wa kampeni uliofanyika eneo la Kwa Pole wilayani hapa huku akiwataka wananchi kutowachagua wagombea wa CCM kwa madai baadhi yao wanatuhumiwa kupokea rushwa.

Akizungumza katika mkutano huo, Nassari alisema pamoja na kuwasilisha ushahidi wake Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ameamua kugawa nakala hizo kuwafungua macho wananchi waelewe kwamba wagombea kutoka CCM hawafai.

Aliwaambia wananchi waliofurika katika mkutano huo ya kwamba wagombea kutoka chama tawala hawastahili kuchaguliwa kwa kuwa baadhi yao walijiuzulu kwa kutuhumiwa kupokea rushwa. Pia alizungumzia kitendo cha baadhi ya wagombea wa CCM kutoa ahadi ya kuyakomboa baadhi ya mashamba yaliyotwaliwa na wawekezaji wilayani humo na kudai kwamba wakati wao wanatoa ahadi jukwaani wao wataingia shambani kudai haki.

“Wakati wao wanaahidi kushughulika na nyaraka sisi watatukuta shambani tunaendelea na kazi sawa,” alisema Nassari.

Mbunge wa Bunda, Bulaya alisema miongoni mwa mambo anayojivunia kwa sasa ni kuondoka CCM na kuhamia upinzani.

Alisema akiwa mwanamke amethubutu kuhamia upinzani kisha kugombea nafasi ya ubunge wa jimbo na hatimaye kulinyakua na kuwataka wanawake kutoogopa na kuwa na uthubutu.

Awali, mgombea udiwani wa kata hiyo, Mollel alisema miongoni mwa vipaumbele vyake pindi atakapopewa ridhaa ni kupigania rasilimali ardhi.

Alisema anawashangaa baadhi ya wagombea kusimama jukwaani kuahidi kukomboa ardhi hiyo huku wakishindwa kujua taratibu za kutwaa ardhi ya wananchi iliyochukuliwa na wawekezaji.