Nassari ashtakiwa kwa kosa la mwaka 2014

Mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki (Chadema) Joshua Nassari, akiwa  na Wakili wake Sheki Mfinanga, katika  Mahakama ya Wilaya ya Arumeru jana. Picha Mussa Juma

Muktasari:

  • Mwendesha mashtaka wa Serikali, Fortunatus Muhalila alidai mbele ya Hakimu Jasmine Abdul kuwa Nassari alimshambulia Neeman Ngudu Desemba 14, 2014.

Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Arumeru kujibu shtaka la shambulio.

Mwendesha mashtaka wa Serikali, Fortunatus Muhalila alidai mbele ya Hakimu Jasmine Abdul kuwa Nassari alimshambulia Neeman Ngudu Desemba 14, 2014.

Anadaiwa kumpiga mateke Ngudu wakiwa katika eneo la Makiba na kumsababishia maumivu akijua kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.

Muhalila alidai kuwa upelelezi wa shauri hilo haujakamilika na kuiomba Mahakama kupanga siku nyingine ya shtaka hilo kutajwa.

Nassari anayetetewa na wakili Sheki Mfinanga alikana kutenda kosa hilo.

Hakimu Jasmine aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 6 itakapotajwa.

Nassari alidhaminiwa na diwani wa Ambuseri, Gabriel Mwanda aliyesaini hati ya Sh5 milioni.

Maduka yawavuruga madiwani

Wakati Nassari akifikishwa mahakamani, Polisi mkoani Arusha juzi jioni walilazimika kuingilia kati kuzima vurugu katika kikao cha madiwani wa Jiji la Arusha waliokuwa wakilumbana kutokana na mgogoro wa umiliki wa maduka 396 ya halmashauri yaliyopo eneo la kituo cha magari.

Katika patashika hiyo, walimkamata diwani wa Daraja Mbili (Chadema), Prosper Msofe aliyeibua hoja ya kumtuhumu meya wa jiji hilo (Chadema), Kalist Lazaro kwamba amekiuka maagizo ya baraza kwa kusaini mkataba uliorejesha maduka hayo kwa watu wanaodaiwa kuyajenga.

Hoja ya Msofe iliyoungwa mkono na diwani wa Ngarenaro (Chadema), Isaya Doita ilipingwa na meya hivyo kuzua malumbano.

Meya Lazaro alisema hajasaini mkataba na kwamba umechukuliwa ofisini kwake kabla hajaufanyia kazi jambo ambalo ni sawa na kuiba nyaraka za Serikali.

Mzozo baina yao uliulazimu uongozi wa jiji kuwaita polisi ambao walimkamata Msofe.

Akizungumzia mgogoro huo, Doita alisema anazo taarifa za kuandaliwa mkataba batili ambao umesainiwa kati ya waliojenga maduka hayo na jiji kinyume cha maagizo ya baraza la madiwani na kamati ya fedha na uchumi.

Alisema msimamo wa kamati na madiwani ni kuwa zabuni itangazwe upya na watakaoshinda ndio wapangishwe maduka.

Juhudi za Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Athuman Kihamia kuwataka madiwani kuwa watulivu na kusikiliza kwa makini hoja kuhusu suala hilo hazikufanikiwa hadi polisi walipoingilia kati na kumkamata Msofe kwa tuhuma za kuiba nyaraka. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo alisema Msofe alishikiliwa kwa mahojiano na baadaye alipata dhamana na uchunguzi wa tukio hilo unaendelea.