Nay wa Mitego kukutana na JPM Ikulu

Msanii wa muziki wa kizazi kipya Emmanuel Elibariki maarufu kama Nay wa Mitego

Muktasari:

Nay amepata mwaliko huo ikiwa ni sasa chache baada ya kuachiwa huru na Jeshi la Polisi lililokuwa likimshikilia tangu jana.

Dar es Salaam.Msanii wa muziki wa kizazi kipya Emmanuel Elibariki maarufu kama Nay wa Mitego ameitwa Ikulu jioni hii kwa ajili ya kufanya mazungumzo na Rais John Magufuli.

Nay amepata mwaliko huo ikiwa ni sasa chache baada ya kuachiwa huru na Jeshi la Polisi lililokuwa likimshikilia tangu jana.

Katika mahojiano yake na kituo cha Televisheni cha Azam Two,  Nay alikiri kupata mwaliko huo na kueleza kuwa ataitumia vyema nafasi hiyo kumuelezea Rais Magufuli hali halisi ya maisha ya Watanzania.

“Nimepokea mwaliko bado nafikiria nini cha kuongea naye endapo nitapata hiyo nafasi ya kuzungumza naye, nadhani itakuwa nafasi nzuri ya kumweleza vile ambavyo Watanzania sisi tunaishi mtaani,”alisema.

Nay alikamatwa na polisi jana mkoani Morogoro na kusafirishwa hadi Dar es Salaam kwa kile kilichodaiwa kutunga wimbo wenye maudhui yanayoikashifu Serikali.

Mapema leo mjini Dodoma, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk Harrison Mwakyembe alisema Rais Magufuli ameagiza msanii huyo aachiwe huru na wimbo wake uendelee kuchezwa na kusambazwa.