Nchemba amvaa Lissu mchanga wa Acacia

Muktasari:

  • Ingawa Mwigulu hakumtaja jina Lissu moja kwa moja alipokuwa akiwahutubia wananchi wa Kijiji cha Zinzirigi kilichopo katika Jimbo lake la Iramba Magharibi pia mkoani Singida juzi, hoja nyingi alizogusia ni zile ambazo Lissu amekuwa akinukuliwa kuzisema.

 Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba ‘amemvaa’ Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu kwamba amejaribu kutengeneza kila aina ya kichaka kukwamisha jitihada za Rais John Magufuli kupambana na usafirishaji holela wa madini nje ya nchi bila mafanikio.

Ingawa Mwigulu hakumtaja jina Lissu moja kwa moja alipokuwa akiwahutubia wananchi wa Kijiji cha Zinzirigi kilichopo katika Jimbo lake la Iramba Magharibi pia mkoani Singida juzi, hoja nyingi alizogusia ni zile ambazo Lissu amekuwa akinukuliwa kuzisema.

Moja ya hoja hizo ni ile ambayo Mwigulu alisema watu wenye nia mbaya walianza kusema kuwa Serikali itashtakiwa kwa hatua yake ya kuzuia makontena 277 ya mchanga wenye dhahabu.

“Baadaye watu haohao walisema tena kwamba mchanga ule ni takataka tu lakini walipoambiwa wasisafirishe mchanga huo wenye madini walisema wanapata hasara ya Sh4 trilioni kwa siku.”

Hata hivyo, Acacia walisema wanapata hasara ya dola bilioni moja kila siku.

Pia, Mwigulu alisema tangu Rais Magufuli alipounda kamati mbili kufuatilia suala la mchanga huo wa madini, watu hao aliowaita kuwa ni wenye nia mbaya walianza kutumia majina ya marais wastaafu Jakaya Kikwete na Benjamin Mkapa kama kichaka ili Serikali iache kufuatilia sakata hilo la mchanga wa madini.

“Hawa watu walikuwa wanatuona kama mazuzu hivi. Rais wetu amechukua hatua tena siyo kwa maneno, kwa vitendo. Tumuunge mkono,” alisema Mwigulu.

Tangu kuanza kwa sakata hilo la mchanga wa madini, Lissu amekaririwa mara kwa mara akisema kwamba suala hilo linashughulikiwa kisiasa badala ya kisheria jambo linaloiweka Tanzania katika hatari ya kushtakiwa na kushindwa.

Pia alikaririwa bungeni akisema Rais Kikwete anaponaje katika sakata hilo na jana alipoulizwa kuhusu kauli hiyo ya Nchemba alisema msimamo wake uko palepale kuhusu sakata hilo.

Alichosema Mwigulu

Mwigulu aliwaeleza wananchi hao kwamba viongozi wa Tanzania hawajawahi kuwa mawakala wa wale wanaoliibia Taifa na kwamba Watanzania wamewaona mawakala wa wezi hao kwa sababu wanawatetea. “Na mimi nimpongeze Rais kwa kuuona ule mtego, akafyatua pyaa! Sasa hivi kama ni gari lao matairi yote, Rais kashayaondoa upepo, yameshalala chini. Maana lile walitaka kutengeneza mtego, yaani ni kama mtu anayepigwa anatafuta mti ili ajifiche,” alisema Mwigulu.

Alisema heshima ya nchi hii kwa viongozi wastaafu waliofanya kazi nzuri ndiyo inayowafanya viongozi wa Taifa hili wasing’ang’anie madarakani, jambo ambalo mataifa mengine wameshindwa kufanya.

“Kama leo una uhakika ukiondoka madarakani unashtakiwa, kwa nini uondoke madarakani?” alihoji Mwigulu na kusisitiza kwamba alichofanya Rais Magufuli ni kulinda heshima za viongozi wastaafu.

Aliwataka wananchi kuunga mkono jitihada za Rais Magufuli za kulinda rasilimali za Taifa kwa sababu ndiyo zinazowawezesha kuwapatia maji, barabara za lami, umeme, elimu bure na dawa.

Lissu ajibu

Akizungumzia kauli ya Mwigulu kwamba wanajificha kwenye kichaka cha viongozi wastaafu ili kufifisha jitihada za Rais Magufuli, Lissu alisema ni ukweli ulio wazi kwamba huwezi kuwataja wahusika wa mikataba mibovu ya madini bila kurudi nyuma.

“Tunawaacha kwa sababu hatuwawezi. Kwa sababu wana kinga,” alisema Lissu na kusisitiza kwamba wanataka kuona wanapata chanzo halisi cha uzembe uliofanyika na siyo kuonea watendaji wadogo.

Lissu alisema Sheria za Madini na mikataba mingi ilisainiwa miaka ya 1997 na 1998.

Lissu ambaye pia ni Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, alieleza kushangazwa na Serikali kuacha kuzungumzia kwamba kampuni ya Acacia haijasajiliwa badala yake Rais Magufuli amekubali kukaa na wale anaowaita wezi ili kujadiliana.

Hatua zilizochukuliwa

Tangu sakata la mchanga wa madini lilipoanza, Rais Magufuli amechukua hatua kadhaa ikiwa ni pamoja na kutengua uteuzi wa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, Bodi ya Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) na ofisa mtendaji mkuu wake na kuagiza viongozi na watendaji wengine kuchunguzwa na vyombo vya dola.

Ripoti ya kamati ya pili iliyoongozwa Profesa Nehemiah Osoro imewataja baadhi ya viongozi waliohusika katika kuingia mikataba tata na kupendekeza Serikali iwachukulie hatua.

Waliotajwa kwenye taarifa ya kamati ya pili iliyowasilishwa kwa Rais Magufuli Juni 12 ni waliokuwa mawaziri katika Wizara ya Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo, William Ngeleja, Nazir Karamagi, Daniel Yona na Dk Abdallah Kigoda ambaye kwa sasa ni marehemu.

Wengine ni waliokuwa wanasheria wakuu, Andrew Chenge na Johnson Mwanyika; manaibu wanasheria wakuu Felix Mrema na Sazi Salula; makamishna wa madini, Paulo Masanja, Dk Dalaly Kafumu na Ally Samaje na wakuu wa idara ya mikataba, Maria Ndosi Kejo na Julius Malaba.

Akizungumzia kutajwa kwake katika ripoti ya kamati ya pili, Mbunge wa Sengerema (CCM), William Ngeleja alisema bungeni kwamba “kutuhumiwa siyo kukutwa na hatia, maisha yanaendelea.”

Viongozi wengine waliotajwa katika ripoti hiyo hawajajitokeza kuzungumzia suala hilo.