Nchi 24 duniani zataka asali kutoka Tanzania

Muktasari:

Tanzania inatajwa kuwa nchi ya pili duniani kwa uzalishaji wa asali ambapo huzalisha tani 38,000 kwa mwaka huku ikichuana na Ethiopia inayozalisha tani 50,000.

Watanzania wamehimizwa kufuga nyuki kwa wingi ili kukuza uchumi kwa kutumia fursa ya upatikanaji wa asali na nta baada ya kuwapo kwa uhakika wa soko la nje kutokana na nchi zaidi ya 24 duniani kuagiza zao hilo.

Tanzania inatajwa kuwa nchi ya pili duniani kwa uzalishaji wa asali ambapo huzalisha tani 38,000 kwa mwaka huku ikichuana na Ethiopia inayozalisha tani 50,000.

Akizungumza katika ofisi za Kampuni ya Mwananchi Communications (MCL) juzi, Meneja Mawasiliano wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Glory Mziray alisema mahitaji ya asali duniani ni makubwa kuliko uzalishaji ulipo. “Hii ni fursa, hivyo Watanzania hatuna budi kuitumia kwa sababu mahitaji huko duniani ni makubwa. Zipo nchi zimetuagiza, lakini bado hatujaweza kukidhi mahitaji ya soko hilo,”alisema.

Mziray alisema uzalishaji wa asali uko chini na kuwa, kwa sasa Tanzania inaweza kusafirisha asilimia 10 ya asali nje ya nchi huku asilimia 90 ikitumika nchini.

Alizitaja nchi zinazohitaji zao hilo kwa wingi kuwa ni Afrika Kusini, India, Botswana, Namibia, Canada, Dubai, Kuwait, Irak, Iran, Japan, China na Lebanon.

Nchi nyingine zinazotaka asali na nta ni Saudi Arabia, Oman Rwanda, Uganda, Kenya, Ufaransa, Uholanzi, Norway, Ujerumani na Uingereza, Marekani na Ireland.

Alisema wastani wa pato linalotokana na nta kwa mwaka ni Sh2.6 bilioni wakati asali ni Sh818.4 milioni na kwamba, linaweza kuongezeka kama uzalishaji utaongezeka.

Ofisa Mawasiliano wa TFS, Tulizo Kilaga alisema ufugaji wa nyuki ni fursa ya uwekezaji ambayo haijachangamkiwa sana na Watanzania, hivyo ni vyema wakachangamka hivi sasa ili waweze kufanikisha masuala yao ya kiuchumi.

Kwa upande wake, Msaidizi wa Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Caroline Mziray alisema ujio wa maofisa wa TFS katika ofisi hizo ulitoa fursa ya kujifunza mambo mbalimbali kuhusu ufugaji wa nyuki na faida kubwa iliyomo katika asali.