Ndege ya kwanza ya ATCL yatua nchini

Moja ya Ndege mpya mbili zilizonunuliwa na serikali kwa ajili ya kampuni ya ndege Tanzania (ATCL) ikiwasili katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere  saa sita na robo juu alama leo Septemba 20, 2016.  PICHA NA IKULU

Muktasari:

Ndege hiyo aina ya Bombadier Q400 NextGen imetua majira ya saa 6:15 mchana na kisha kupatiwa heshima maalum ambayo hutolewa kwa ndege yoyote mpya inayotua katika nchi yake (Water Salute).

Dar es Salaam. Ndege mpya ya kwanza iliyonunuliwa na Serikali kwa ajili ya kutumiwa na Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) imetua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam ikitokea nchini Canada ilikotengenezwa.

Ndege hiyo aina ya Bombadier Q400 NextGen imetua majira ya saa 6:15 mchana na kisha kupatiwa heshima maalum ambayo hutolewa kwa ndege yoyote mpya inayotua katika nchi yake (Water Salute).

Baada ya kupokea heshima hiyo, ndege imeegeshwa katika eneo la ndege za jeshi (Airwing Ukonga).

Akizungumza baada ya kuwasili kwa ndege hiyo Katibu Mkuu Uchukuzi Dk Leonard Chamriho amesema ndege ya pili inatarajiwa kuwasili baada ya wiki moja na kwamba baada ya kuwasili ndege ya pili ndipo yatafanyika mapokezi rasmi, yatakayoongozwa na Rais John Magufuli kwa tarehe itakayotangazwa baadaye.