Friday, July 21, 2017

Ndoa ya aina yake yafungwa Dar

 

By Prosper Kaijage, Mwananchi pkaijage@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Hayawi hayawi sasa yamekuwa, ndivyo unavyoweza kusema, baada ya Asha Abdallah maarufu Binti Dulla anayesadikiwa kuwa na umri wa zaidi ya miaka 60, mkazi wa Mburahati Madoto kuolewa na Ally Kimbunga (35).

Ndoa hiyo ilifungwa jana saa saba mchana nyumbani kwa Binti Dulla ikishuhudiwa na watu wengi ambayo ilitanguliwa na sherehe iliyoambatana na ngoma siku mbili kabla ya kufungwa.

Ndugu katika familia ya bibi harusi, Hamisi Kondo alimwambia mwandishi wetu kuwa hiyo ilikuwa ni ndoa ya nne kwa dada yake na kwamba, waliomuoa awali walishafariki dunia.

“Sasa hivi hana watoto, aliwahi kuwa na mmoja ila ikawa si riziki kwa kuwa alifariki akiwa na miaka mitatu,” alisema Kondo ambaye mama wa Binti Dulla ni shangazi yake.

Kudra Saidi aliyewahi kuwa mpangaji nyumbani kwa Binti Dulla kwa miaka 12 tangu 1990 ambaye alihudhuria ndoa hiyo alisema majirani walipomfuata kuzungumza naye kuhusu kuolewa aliwaeleza kuwa hata Mtume Muhammad (SAW) alioa mwanamke aliyemzidi umri.

Kudra alisema baadhi ya watu wamekuwa wakidai kwamba mume wa Binti Dulla amefuata nyumba na kwamba mama huyo hana haja ya kupata mtoto.

Hata hivyo, Binti Dulla alisema maneno yanayozungumzwa kuhusu ndoa yake ni wivu wa baadhi ya watu katika maisha aliyoyachagua.

“Wazushi tena hao ni mashilawadu (wambeya) kwa kuwa walijua sitafanikisha. Kuhusu suala la mtoto sina haja ya kupata mtoto kwa kuwa nia yangu ni kuolewa na kuwa na mume, Mungu amefanikisha hilo, Alhamdulillah Rabil-alamin,” alisema Binti Dulla.

Binti Dulla alisema mama yake hakufika kwenye ndoa yake kwa kuwa ni mgonjwa na anasumbuliwa na maradhi ya moyo.

“Mama yangu hakufika kutokana na hali yake na hayupo hapa anaishi Bagamoyo. Juzi alitoka hapa kwangu alikokuwa akipatiwa matibabu, isingekuwa rahisi kwa yeye kuja,” alisema.

Akizungumzia ndoa hiyo mume Kimbunga alisema yeye si wa kwanza kuoa mtu aliyemzidi umri. Alisema anamshukuru Mungu kwa hatua aliyopiga, huku akisema wanaozungumza anawaacha waongee kwa kuwa ameshazoea.

“Sikuanza naye jana wala juzi, niko naye tangu mwaka 2007. Sijawahi kuoa na ndiyo mara yangu ya kwanza na nimefuata maadili ya dini yangu na sunna ya Mtume Muhammad (SAW) ambaye alioa mwanamke aliyemzidi umri,” alisema Kimbunga.

Alisema wanaodai yuko naye kwa ajili ya masilahi ni wazushi na kwamba, mke wake ni mgonjwa wa kisukari tangu walipokutana na kama kumuacha angemucha kipindi cha nyuma lakini wanapendana.

Kimbunga alisema licha ya kuwa ni ndoa yake ya kwanza, ana mtoto wa kike mwenye miaka 15 ambaye alikuwapo kwenye harusi.

Alisema mama yake anaishi Morogoro na kwamba, mzazi mwenzake hana shida juu ya yeye kuoa.

Jirani wa Binti Dulla (jina linahifadhiwa) aliyehudhuria ndoa hiyo na sherehe hizo za siku mbili alisema ni vyema maharusi hao wangefunga ndoa kimyakimya kutokana na umri wa mke.

-->