KESI MAUAJI YA BILIONEA MSUYA-Ndugu waangua kilio mahakamani

Mawakili wa utetezi katika Kesi ya mauaji ya mfanyabiashara wa Madini ya Tanzanite Erasto Msuya wakiwa katika  Chumba cha Mahakama Kuu Kanda ya Moshi jana, Kabla kesi ya kuanza. Picha na Dionis Nyato

Muktasari:

  • Hali hiyo ilijitokeza jana saa 4:55 asubuhi wakati shahidi wa 27 wa upande wa mashtaka, mkaguzi wa polisi, Damian Chilumba alipoonyeshwa kielelezo cha bunduki hiyo ili aweze kuitambua mahakamani.

Bunduki aina SMG inayodaiwa kutumika kumuua mfanyabiashara, Erasto Msuya, imesababisha kilio kwa dakika kadhaa mahakamani kwa mdogo wa marehemu, Bahati Shujaa baada ya kuiona silaha hiyo.

Hali hiyo ilijitokeza jana saa 4:55 asubuhi wakati shahidi wa 27 wa upande wa mashtaka, mkaguzi wa polisi, Damian Chilumba alipoonyeshwa kielelezo cha bunduki hiyo ili aweze kuitambua mahakamani.

Baada ya kuitoa bunduki hiyo kutoka mfuko wa sandarusi, mdogo wa marehemu na mwanafamilia mwingine, Lightness Lawrence walianza kuangua kilio kwa sauti ya chini.

Hata hivyo, mkaguzi msaidizi wa polisi aliyetajwa kwa jina la Msuya, alitoa ishara ya kuondolewa ndani kwa wanafamilia hao.

Polisi wa kike aliyekuwapo ndani ya mahakama, aliwafuata ndugu hao na kuwatoa nje. Hata hivyo, walipovuka tu mlango wa mahakama ya wazi, Bahati alilia kwa sauti ya juu hali iliyowafanya askari waliokuwapo nje kuwaondoa eneo hilo.

Wakati shahidi huyo akiendelea kutoa ushahidi wake mbele ya Jaji Salma Maghimbi, akiongozwa na wakili wa Serikali mwandamizi, Abdallah Chavulla, ndugu hao walirejea mahakamani saa 5:10 asubuhi.

Tukio kama hilo lilitokea Februari 8, dada mwingine wa marehemu, Antuja Msuya alipoangua kilio mahakamani baada ya kuiona bunduki hiyo ya kijeshi yenye namba 1952 r KJ 10520.

Akiendelea kutoa ushahidi wake jana, Chilumba alidai ni miongoni mwa makachero walioshiriki kuitafuta SMG hiyo inayodaiwa kufichwa kichakani na mshtakiwa wa sita, Sadick Jabir.

Alipoulizwa na Chavulla vitu vitakavyomsaidia kuitambua bunduki hiyo, shahidi huyo alidai ataitambua kwa aina yake ya SMG, uchakavu na namba zake ambazo ni 1952 r KJ 10520.

Baada ya kueleza hivyo, Chavulla alimpa mfuko wa sandarusi ambao ndani yake kulikuwa na bunduki hiyo, akimtaka aufungue kisha aiambie Mahakama kitu kilichomo ndani.

Alipoikagua namba zake, shahidi huyo alimweleza Jaji Maghimbi kuwa bunduki hiyo ndiyo iliyopatikana katika matindiga huko Sanya Juu kwa maelekezo yanayodaiwa ni ya mshtakiwa Jabir.

Shahidi huyo alidai baada ya kukamilika kwa kazi ya kutafuta bunduki hiyo, walielekea Bomang’ombe wilayani Hai kuchukua moja ya pikipiki zinazodaiwa kutumika katika mauaji hayo.

Pikipiki hiyo aina ya King Lion rangi nyeusi namba T751 CKB, inaelezwa mshtakiwa huyo anadaiwa kuwaelekeza polisi wamtafute ndugu yake aitwaye Adam Jabir anajua ilipohifadhiwa.

Katika ushahidi wake, shahidi huyo wa 27 wa Serikali alidai kuwa baada ya kumpata Said, aliwaeleza kuwa pikipiki hiyo alikuwa ameihifadhi kwa mfanyabiashara aitwaye Mahmoud Shaaban.

Kwa mujibu wa shahidi huyo, baada ya kufika nyumbani kwa mfanyabiashara huyo katika mji wa Bomang’ombe, waliipata pikipiki hiyo na kuichukua baada ya kujaza hati ya polisi ya upekuzi na makabidhiano.

Shahidi huyo aliiomba mahakama ipokee hati hiyo ya makabidhiano ya pikipiki hiyo kama kielelezo, ombi ambalo lilipingwa na jopo la mawakili wanne wa utetezi likiongozwa na Majura Magafu.

Hoja za utetezi

Akitoa hoja za kupinga kupokewa kielelezo hicho, Magafu alidai hati hiyo inaonyesha mmiliki wa pikipiki hiyo ni Said Jabir na mashahidi ni Shaaban Mahmoud na Jamal Othant.

“Kwa mujibu wa ushahidi wake Damian Shilumba (shahidi wa 27), pikipiki ilikutwa kwa Shaaban Mahmoud. Kwa ushahidi wake anadai aliyeipeleka kwa Shaaban ni Said Mohamed Jabir,” alidai Magafu na kuongeza:

“Hawa watu wawili Said na Shaaban si washtakiwa kwenye hii kesi. Said hatujui yuko wapi ili sasa aje atuthibitishie kuwa ni kweli ndiye aliyewapeleka polisi kwa Shaaban.

“Shaaban hajafika yeye kama yeye kutoa ushahidi wake mahakamani, badala yake statement (maelezo) yake ndiyo imesomwa mahakamani baada ya upande wa mashtaka kudai hapatikani.”

Magafu alidai ili hati hiyo ya makabidhiano iweze kupokewa na mahakama kama kielelezo cha kesi, lazima iwe halali (authentic) na kuthibitisha hilo lazima waliosaini waletwe.

Alidai kwa mujibu wa sheria, ili hati hiyo iweze kupokewa kortini kama kielelezo, lazima isainiwe na makundi matatu ambayo ni pamoja na aliyekuwa akiimiliki pikipiki hiyo.

“Aliyekutwa anaimiliki kwa mujibu wa nyaraka hii Said Mohamed Jabir, lakini kwa ushahidi wake (shahidi wa 27) pikipiki hii ilikutwa kwa Shaaban. Nani atatuthibitishia haya?

“Kundi la pili ni la mashahidi walioushuhudia upekuzi ukifanyika, lakini swali la kujiuliza linalotakiwa kujibiwa na Mahakama ni nani alikutwa na pikipiki kati ya Said na Shaaban?

“Unapokosekana ushahidi wa Said ni rai yetu kuwa tunabaki njia panda. Kama ndivyo, mahakama itaamini Shaaban alikuwa ni mshuhudiaji tu wala si shahidi wa upande wa mashitaka.

“Jambo lingine, ni kuwa document (nyaraka) inapotakiwa kutolewa kama kielelezo, inatakiwa ithibitishe kesi dhidi ya washtakiwa waliopo kizimbani,” alidai Magafu na kuongeza:

“Said anayetajwa kuwa ndiye alikuwa akiimiliki si mshtakiwa katika kesi hii. Shaaban ambaye pikipiki ilikutwa kwake japo anasema ililetwa kwake na Said, naye si mshtakiwa katika kesi hii.”

Pia, Magafu alidai sheria inayosimamia upekuzi inataka upekuzi ufanywe na ofisa mfawidhi wa kituo cha polisi na katika mazingira ya siku hiyo alipaswa kuwa SP Vincent Lyimo.

“Sheria inataka aende yeye mwenyewe kwa discretion (utashi wake), kama hataenda yeye atamtuma ofisa mwingine kwa maandishi. Shahidi wa 27 hakuna ushahidi alikoteuliwa kuendesha upekuzi huo,” alidai.

Majibu ya Jamhuri

Akijibu hoja hizo, Chavulla anayesaidiana na mawakili wa Serikali, Kassim Nassir na Ignas Mwinuka, alidai kuwa wao hawakubaliani na hoja za mawakili hao akisisitiza kuwa hazina mashiko.

Chavulla alidai mawakili wa utetezi walidai ni lazima anayepaswa kufanya upekuzi awe ofisa mfawidhi wa kituo cha Polisi na kwamba, hiyo ni tafsiri potofu kwa kuwa sheria haikuweka takwa la lazima.

Kuhusu waliosaini hati hiyo (Said na Shaban) kutokuwa washtakiwa katika kesi hiyo, Chavulla alidai kuwa haijasema lazima wawe washtakiwa bali inataka awe mmiliki au aliyeihifadhi.

“Kesi iliyopo mbele yako mheshimiwa Jaji ni mauaji ya Erasto Msuya yaliyofanyika Agosti 7, 2013 eneo la Mijohoroni wilayani Hai. Hilo halina ubishi kuwa ndiyo kesi iliyopo mbele yetu,” alieleza Chavula na kuongeza:

“Katika mauaji hayo kinachobishaniwa ni kuwa waliotekeleza mauaji hayo walitumia pikipiki mbili na moja ni T751 KCB King Lion nyeusi.

“Pikipiki hiyo imepatikana kwa Shaaban Mahmoud na aliyewezesha kupatikana kwake ni miongoni mwa washtakiwa (Sadick Jabir). Kwa hiyo kielelezo kina uhusiano na kesi hii.”

Baada ya kusikiliza mabishano hayo ya kisheria, Jaji Maghimbi aliahirisha kesi hiyo saa 7:15 mchana hadi saa 9:00 alasiri, ili aweze kupata muda wa kuandaa uamuzi mdogo wa mabishano hayo.

Uamuzi wa Mahakama

Katika uamuzi wake mdogo, Jaji Maghimbi alitupilia mbali mapingamizi ya upande wa utetezi na kuamua hati hiyo ipokewe kama kielelezo cha kesi hiyo kwa kuwa kina uhusiano na tukio hilo la mauaji na kiliandaliwa na shahidi huyo wa 27.

Baada ya uamuzi, Chavulla aliiomba mahakama iahirishe kesi hiyo hadi kesho itakapoendelea kusikiliza ushahidi wa shahidi huyo wa 27, kwa kuwa ushahidi wake bado ni mrefu.