Ndugu wagoma kuzika mwili wa anayedaiwa kuuawa na askari wa mgodi Geita

Muktasari:

Familia ya Mengineyo Mabula, mkazi wa Samina anayedaiwa kuuawa na walinzi wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM)  wamegoma kuuzika mwili wa ndugu yao hadi mgodi utakapokubali kugharamia mazishi.

Mengineyo anadaiwa kupigwa risasi na walinzi wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita

Geita. Familia ya Mengineyo Mabula, mkazi wa Samina mjini Geita anayedaiwa kuuawa na walinzi wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) usiku wa kuamkia juzi, wamegoma kuuzika mwili wa ndugu yao hadi mgodi utakapokubali kugharamia mazishi.

Mengineyo anadaiwa kupigwa risasi na askari hao alipoingia kwenye mgodi huo kwa njia za panya kwa lengo la kuiba mawe yanayodhaniwa kuwa na dhahabu

Hata hivyo, wakati polisi mkoani Geita wakisema walinzi wa GGM walilazimika kutumia silaha za moto kupambana na wavamizi, meneja mawasiliano na uhusiano wa mgodi huo, Tenga Tenga alisema walinzi wao hawatumii silaha za moto na jambo hilo bado linachunguzwa.

Familia inasemaje?

Msemaji wa familia, Deus Daniel alisema licha ya ndugu yao kudaiwa kuingia mgodini kwa njia za panya, hatua iliyochukuliwa kumuondolea uhai ni kubwa, hivyo ni wajibu wa mgodi kugharamia mazishi. “Tumeshakutana nao, wao ndiyo chanzo cha kifo cha ndugu yetu hata kama aliingia kwa njia haramu, lakini adhabu waliyoichukua ni kubwa, sisi tunatulia, hatuziki,” alisema Daniel. Wao ndiyo wameua halafu wanataka tuandike barua kuwaomba (msaada wa kugharimia mazishi).”

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo alisema mauaji hayo yalitokea juzi saa tisa usiku wakati Mabula alipoingia mgodini kwa njia za panya kwa lengo la kuiba mawe yanayodhaniwa kuwa na dhahabu.

Mwabulambo alisema kuwa Mabula akiwa na wenzake tisa, waliingia mgodini katika eneo la Nyankanga linalolindwa na walinzi wa GGM pamoja na askari polisi, na walinzi wa mgodi walilazimika kutumia silaha za moto kutokana na upinzani waliokabiliana nao. “Katika kudhibiti ndipo risasi zilimpata (Mengineyo) sehemu ya kifuani na tumboni na sasa tunachunguza risasi hizo ni za silaha ya aina gani na tunawashikilia watu tisa waliovamia mgodi pamoja na viroba viwili vya mawe yanayodhaniwa kuwa na dhahabu yaliyokutwa katika eneo hilo,” alisema

Hata hivyo, kamanda huyo alisema wanawashikilia walinzi watatu wa mgodi kwa mahojiano na uchunguzi wa tukio hilo unaendelea.

Wanachosema GGM

Wakati polisi ikisema walinzi wa GGM walilazimika kutumia silaha za moto kukabiliana na wavamizi, meneja mawasiliano na uhusiano wa GGM, Tenga alisema, “Kwa masikitiko makubwa tumepokea taarifa ya mauaji na GGM tunasikitika sana kwa kifo hicho, jambo hilo lipo kwenye uchunguzi hatuwezi kuzungumzia mpaka uchunguzi utakapokamilika.”

Alipoulizwa na Mwananchi iwapo askari wao wanatumia silaha za aina gani, alisema hawatumii silaha za moto na kwamba, hakuna namna yoyote ambayo GGM wanaweza kufanya mauaji na kudai uchunguzi wa polisi utakuja na majibu sahihi.

Siyo tukio la kwanza

Tukio hilo la mauaji ni la pili ndani ya mwezi mmoja. Mwanzoni mwa mwezi huu, mkazi mwingine wa mjini Geita alidaiwa kuuawa na walinzi wa mgodi huo.

Shida Lugesha, ambaye ni mjumbe wa mtaa huo, alisema sababu kubwa inayowafanya vijana kuingia mgodini ni hali ngumu ya maisha, baada ya wakazi hao kutokuwa na eneo la kilimo wala la uchimbaji madini.