Ndugu wakataa kuchukua mwili wa Akwilina Muhimbili

NDUGU WA AKWILINA WAKUSANYIKA MUHIMBILI KUSUBIRI POSTMORTEM

Muktasari:

Katika madai yao ndugu wa marehemu wanataka wapewe ripoti ya uchunguzi wa kifo hicho kwanza kabla ya kwenda kumzika.


Dar es Salaam.  Dada wa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwiline aliyeuawa kwa kupigwa risasi na polisi, Tegolena Uiso amesema hawatapokea mwili wa mwanafunzi huyo bila kuelezwa nini kilichomuua ndugu yao.

Mwili wa Akwilina umehamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ukitokea Hospitali ya Mwananyamala kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi.

Akizungumza leo Februari 19, 2018 na MCL Digital akiwa MNH, Tegolena amesema ni vyema wakapewa ripoti kuhusu kilichogundulika baada ya ndugu kuelezwa kuwa mochuari ya  Muhimbili kwamba watatoa ripoti ya uchunguzi baada ya siku 14.

"Sisi tumekuja kwa ajili ya kujua hasa ndugu yetu nini kimemkuta hatuwezi kupokea mwili bila ripoti. Wanatuambia  ni baada ya wiki mbili sina hakika kama hawajabaini kitu chochote, hatuwezi kuuchukua mwili mpaka tupewe sababu," amesema Tegolena.

Amesema mpaka sasa wamezungumza na Mkuu wa Chuo cha Usafirishaji NIT, Profesa Zakaria Mhanilwa ambaye bado anawasiliana na madaktari ndani na hawajajua iwapo atakuja na majibu sahihi.

Awali, Profesa Mhanilwa amesema amefika hospitalini hapo kufuatilia uchunguzi huo akiwa ni miongoni mwa wafiwa.

Akwilina alifariki dunia Februari 16, 2018 baada ya kupigwa risasi kichwani akiwa kwenye daladala wakati polisi wakiwatawanya waandamani ambao ni wafuasi wa Chadema.