Ndugulile aupa rungu uongozi kituo cha Nunge

Muktasari:

Ametoa muda wa wiki mbili kumalizwa kwa changamoto ya usafiri kwa wazee

Dar es Salaam. Serikali imeutaka uongozi wa kambi ya wazee na watu wasiojiweza ya Nunge kuwakamata wanaohusika kuuza viwanja katika eneo la kambi hiyo.

Kauli hiyo imetolewa leo Alhamisi Mei 24, 2018 na Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile  wakati akijibu kero za  wazee wa kituo hicho kilichopo Kigamboni jijini Dar es Salaam alipowatembelea.

Sambamba na hilo Dk Ndugulile amesimamisha ujenzi wa nyumba  nje na kambi hiyo  kwa maelezo kuwa uongozi wa kambi hiyo haujui lolote.

“Marufuku kwa mtu yeyote kuuza, kununua wala kujenga  pamoja na kuchimba mchanga katika eneo la kambi hii na mtu atakayebainika anajihusisha na vitendo hivyo basi hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake,” amesema naibu waziri huyo.

Aidha, Dk Ndugulile amesema misaada inayokuja katika kambi hiyo iwekewe utaratibu ili kila mmoja aweze kupata.

Pia, ametoa muda wa wiki mbili kumalizwa kwa changamoto ya usafiri kwa wazee wa kambi hiyo akitaka kukarabatiwa kwa bajaji iliyotolewa na Serikali.

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa kituo cha afya cha kambi ya wazee  Nunge, Dk Dismas Chihwalo amesema, “erikali inatakiwa kuhakikisha wanaoletwa kwa ajili ya huduma maalum wanatia saini mkataba wa makubaliano ili kuepusha migogoro ya kutoa huduma katika kambi hiyo kwa wanaostahili.”

Kambi hiyo  ilianzishwa mwaka 1936 kwa ajili ya kuwahudumia wazee na wasiojiweza.