Thursday, September 14, 2017

Neec, PPRA wakubaliana ununuzi wa umma

 

By Elizabeth Edward, Mwananchi eedward@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (Neec) limeingia makubaliano ya ushirikiano na Mamlaka ya Ununuzi wa Umma (PPRA) kwa lengo la kuongeza ushiriki wa wafanyabiashara wadogo na wa kati katika ununuzi wa umma.

Katibu Mtendaji wa Neec, Beng’i Issa amesema makubaliano hayo yamefikiwa ili kuwavuta zaidi wafanyabiashara wazawa kupata zabuni za ununuzi wa umma.

Amesema kupitia makubaliano hayo baraza litaweza kutatua changamoto za wafanyabiashara hao, ikiwemo kuwajengea uwezo ili waweze kuelewa utaratibu wa kushiriki zabuni.

“Wafanyabiashara wengi hawaelewi fursa zilizopo kwenye mashirika ya umma na utaratibu wa kushiriki zabuni, wanashindwa kutimiza masharti kutokana na kukosa mitaji ya kutosha na mambo mengine yanayowasababisha wakose fursa hizo,” amesema.

Beng’i amesema, “Fursa ambazo zipo kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati katika taasisi za umma ni pamoja na huduma za ukarabati, uuzaji samani na vifaa vya ofisi, huduma za usafi, chakula, ulinzi na nyingine nyingi.”

Ofisa Mtendaji Mkuu wa PPRA, Dk Laurent Shirima amesema taasisi hiyo itahakikisha michakato ya ununuzi inayofanywa na taasisi za umma inaendeshwa katika misingi ya haki, ushindani na uwazi.

Dk Shirima amesema kutakuwa na upendeleo kwa wazabuni wa ndani na wale walio katika makundi maalumu wakiwemo wanawake, vijana, wazee na walemavu.

Amesema kandarasi zinazohusisha zabuni za ununuzi wa vifaa vyenye thamani chini ya Sh2 bilioni zinatakiwa kutolewa kwa wazabuni wa ndani.

-->