Neema ya maji ilivyowashukia wakazi wa Kijiji cha Ngireyani Longido

Muktasari:

  • Kukosekana kwa majisafi na salama katika kijiji hicho ni miongoni mwa kero zilizokuwepo kwa muda mrefu na kusababisha shughuli za maendeleo mbalimbali ya kijiji hicho na hasa zile za kujiingizia kipato kukwama.

Uhaba wa maji katika Kijiji cha Ngireyani wilayani Longido mkoani Arusha ni miongoni mwa changamoto ambazo zimekuwa zikisababisha kero na usumbufu kwa wakazi wa wilaya hiyo hususani kwa kutembea umbali mrefu kusaka huduma ya majisafi huku wakitishiwa kushambuliwa na wanyama wakali.

Kukosekana kwa majisafi na salama katika kijiji hicho ni miongoni mwa kero zilizokuwepo kwa muda mrefu na kusababisha shughuli za maendeleo mbalimbali ya kijiji hicho na hasa zile za kujiingizia kipato kukwama.

Kijiji cha Ngireyani ni miongoni mwa vijiji vichache nchini ambavyo vimekuwa vikikabiliwa na changamoto hiyo kwa muda mrefu kitendo ambacho kimesababisha wakinamama na watoto kuwa katika kundi la kwanza kuathirika kutokana na kuamka usiku kwenda kutafuta majisafi na salama.

Hatahivyo, pamoja na changamoto ya upatikanaji wa majisafi na salama kuendelea kuwepo nchini, Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo nchini wameendelea kufanya uwekezaji mkubwa zaidi kuboresha huduma ya maji vijijini kupitia jitihada na mipango mbalimbali.

Hivi karibuni Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) liligharamia ujenzi wa mradi wa kisima cha maji chenye uwezo wa kuhudumia wakazi zaidi ya 4,000 na mifugo mbalimbali.

Mradi huo umetekelezwa na Shirika la Tanzania Pastoralist Hunters and Gatherers Organization (Taphgo) kwa Sh200 milioni. Kisima hicho kinatumia umeme wa nguvu za jua (solar) kusukuma mitambo ya maji huku kikiwa na uwezo wa kuhifadhi jumla ya lita 10,000 za maji kila siku.

Inaendelea uk 28

Inatoka uk 23

Akizungumza hivi karibuni mara baada ya uzinduzi wa kisima hicho, Ofisa Programu wa Shirika la Taphgo, Joshua Kuney anasema mradi huo ulianzishwa mahsusi kwa ajili ya wakazi wa kijiji hicho ambao wengi wao ni wafugaji.

Anasema awali walianza kuutekeleza mradi huo lakini walibaini kuwa ukosefu wa maji katika Kijiji cha Ngireyani ulikuwa kero kwa wakazi wa eneo hilo hatua iliyowasababishia kufikiria namna ya kutatua changamoto hiyo.

“Tuliona umuhimu wa kuleta mradi huu hapa Ngireyan kwa kuwa eneo hili lina ukame mkali hivyo wananchi na mifugo wanahangaika sana kupata huduma ya maji safi na salama,”anasema Joshua.

Kuney anasema kwamba mradi huo utakuwa na manufaa mbalimbali kwa wakazi wa eneo hilo ambapo mbali na kusaidia kuhifadhi mazingira karibu na kisima hicho lakini wakazi wa eneo hilo watajishughulisha na kilimo cha mbogamboga na upandaji wa miti karibu na eneo hilo.

Kwa upande wake ofisa miradi wa shirika hilo, Joseph Ole Shangai anasema kwa sasa baadhi ya maeneo nchini yamekuwa yakiathiriwa na changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi na hivyo shirika lao limelenga kukabiliana na changamoto hiyo kwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya majisafi na salama.

“Kwa sasa tuna changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi hivyo sisi kama shirika tumelenga kukabiliana na changamoto hii kwa kuhakikisha wananchi wanaoishi maeneo ya vijijini wanapata huduma ya maji safi na salama,” anasema Ole Shangai.

Anasisitiza kwamba mradi huo wa maji unalenga pia matumizi ya binadamu na wameweka bomba la maji katika umbali wa mita 100 kutoka eneo la mradi ambapo wakina mama watayatumia maji hayo kwa ajili ya matumizi yao ya nyumbani kama kufulia,kupikia,kuoshea vyombo na hata kunywa.

Ole Shangai anasema lengo kuu la mradi huo ni kupunguza ule muda wa wananchi kutembea umbali mrefu kusaka huduma ya maji kuutumia katika shughuli mbalimbali za kujiingizia kipato na hata maendeleo yao.

“Hali ya kijiographia katika eneo hili ni kame hivyo wananchi walikuwa wakisafiri umbali mrefu kusaka maji safi na salama, hivyo mbali na matumizi ya nyumbani pia wananchi watayatumia maji haya kwa kilimo cha mbogamboga hatua itakayowaingiza kipato,” anasema Ole Shangai.

Hata hivyo, Ole Shangai anataja miongoni mwa changamoto ambazo walizipata wakati wakianza kuutekeleza mradi huo ni pamoja na tatizo la upatikanaji wa maji wilayani Longido ambapo hapo awali waliwekeza rasilimali kama fedha katika eneo la Tingatinga kuchimba maji lakini mwisho wa siku waliambulia patupu.

“Pamoja na nia yetu njema lakini awali tulihangaika sana kupata maji, tulichimba maji eneo la Tingatinga na hatukupata maji pamoja na kwamba tayari tulikuwa tumeshawekeza rasilimali mbalimbali kama fedha,” anasema Ole Shangai.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa kijiji hicho, Jackson Keriango anasema kwamba awali wananchi walilazimika kutembea umbali wa zaidi ya kilomita 10 wakiongozana na mifugo kusaka huduma ya majisafi na salama.

Keriango anasema kwamba kulikuwa na matukio ya baadhi ya mifugo kuchoka na kushindwa kutembea huku baadhi ya kina mama wajawazito walilazimika kujifungulia njiani wakati wakielekea kusaka huduma ya maji ya kwa ajili ya matumizi mbalimbali majumbani.

Anasema Kijiji cha Keriango kina jumla ya vitongoji vinane na zaidi ya wakazi 4000 wakiwemo wafugaji ambao hutembea umbali mrefu kusaka maji kwa ajili ya mifugo ambapo baadhi ya mifugo ilipatwa ugonjwa wa mapafu kutokana na vumbi njiani.

“Madhara ya wafugaji kutembea na mifugo umbali mrefu ni pamoja na mifugo kushikwa na ugonjwa wa mapafu kutokana na kuvuta vumbi njiani wakati ikipelekwa kusaka maji ya kunywa,” anasema Keriango.

Anasema baadhi ya akinamama walikuwa wakiamka usiku kuanza safari katikati ya mapori kusaka maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani kama kuoshea vyombo, kufulia, kupikia na hata kwa kuoshea watoto wao.

Anaongeza kwamba wao kama uongozi wa Serikali ya kijiji wamejiandaa vyema kuupokea mradi huo na kuutunza kwa hali na mali huku akisisitiza kuwa wamejipanga kuutunza ili uwe faida kwa vizazi vijavyo.

“Natoa wito kwa wananchi kuutunza mradi huu, lazima tudumishe usafi na tuutunze mradi kwa ajili ya vizazi vijavyo,” anasema Keriango.

Naye mwenyekiti wa kitongoji cha Emboreet A, Oloitai Kipara mbali na kuwashukuru wafadhili waliosaidia upatikanaji wa mradi huo pia alisema kwamba kero ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika kitongoji chake ni miongoni mwa kero ambazo zimekuwa zikisababisha usumbufu mkubwa kwa wakazi wa eneo lake.

Kipara anasema kwamba wao kama uongozi ambako mradi unapatikana wamejipanga kuunda kamati ya wazee itakayokuwa na jukumu la kusimamia mradi huo na miongoni mwa majukumu ya kamati hiyo ni pamoja na kupanga utaratibu mzuri wa matumizi ya maji ya mradi huo.

“Tumeteua kamati ya wazee kusimamia mradi huu kamati hii itaweka utaratibu mzuri wa matumizi katika siku zote lengo ni kuuweka katika hali nzuri usiharibike,” anasema Kipara.

Kipara anasema kwamba awali baadhi ya watoto hususani wanafunzi walikuwa wakikatisha masomo na hata wengine kushindwa kuhudhuria masomo shuleni kutokana na kwenda kusaka maji jambo lililopelekea kuathiri masomo yao shuleni.

Meoshi Laiser ambaye ni mkazi wa eneo hilo anasema awali walilazimika kusafiri umbali mrefu na punda kwenda kutafuta maji katika vijiji vya jirani ambapo watoto na wakinamama waliteseka wakiwa njiani.

“Tulikutana na wanyama wakali porini kama tembo au simba na hivyo hata punda tuliokuwa tumeandamana nao walikimbia hovyo na hatukuambulia chochote huko tulikokwenda,” anasema Laiser.

Mkazi mwingine wa eneo hilo, Ngalila Olonyike alisema baadhi ya wanawake walishikwa na uchungu na hata kulazimika kujifungua wakiwa maporini katika harakati za kusaka huduma ya maji safi na salama.

“Tumefurahi sana kupata maji kwa kuwa nakumbuka tulilala maporini kusaka maji wengine tulishikwa na uchungu na hata kulazimika kujifungua tukiwa maporini na tulikosa hata maji ya kuwasafishia watoto wetu,” anasema Olonyike.

Joseph Kitutu ambaye ametoa eneo lake kutumika katika ujenzi wa mradi huo anasema kwamba upatikanaji wa maji katika eneo lao utasaidia kuleta uhai wa binadamu na wanyama katika eneo hilo na kuiomba Serikali kujikita katika kutengeneza miradi mingi ya maji hususani katika maeneo ya vijijini.

“Mke wangu alilazimika kutumia siku mbili safarini tena bila punda wakati akisaka maji hakika tuliteseka sana cha msingi tunaomba Serikali ipanue miradi mingi ya maji hususani katika maeneo ya vijijini,” anasema Kitutu.

Naye Londoye Pariti, ambaye ni kiongozi wa vijana wa kimasai katika eneo hilo maarufu kama morani anasema kwamba wao kama vijana wamejipanga kuhakikisha wanaimarisha ulinzi katika eneo la mradi huo.

“Tunamshukuru Mzee Kitutu kwa kutupatia eneo hili kutumika kama eneo la mradi sisi kama vijana wa kimasai tumejipanga kuhakikisha tunaimarisha ulinzi katika eneo hili ili kuufanya mradi uwe endelevu,” anasema Pariti.