Ng’ombe 4,678 wakamatwa ndani ya hifadhi

Muktasari:

Mhifadhi Mkuu wa Kanda ya Magharibi Kituo cha Handajega, Robert Mduma alisema wamiliki wa mifugo hiyo wametozwa faini ya Sh23.3 milioni kwa gharama ya Sh5,000 kwa kila ng’ombe.  

Busega. Ng’ombe 4,678 wamekamatwa wakilishwa ndani ya Pori la Akiba la Kijereshi ikiwa ni utekelezaji wa amri ya Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Ramo Makani aliyeagiza mifugo yote kuondolewa ndani ya hifadhi hiyo.

Mhifadhi Mkuu wa Kanda ya Magharibi Kituo cha Handajega, Robert Mduma alisema wamiliki wa mifugo hiyo wametozwa faini ya Sh23.3 milioni kwa gharama ya Sh5,000 kwa kila ng’ombe. 

“Wafugaji hao walikuwa wakiwatumia watoto kuchunga mifugo ndani ya eneo la hifadhi kinyume na sheria. Licha ya kuvunja sheria za uhifadhi zinazozuia shughuli za kibinadamu ndani ya maeneo yaliyohifadhiwa, wazazi hawa pia walikuwa wanahatarisha maisha ya watoto wao ambao wangeweza kushambuliwa na wanyama wakali porini,” alisema Mduma.