Sunday, November 19, 2017

VIDEO-Watendaji waonywa kuhusu mifugo katika maeneo yao

By By Rajabu Athumani, Mwananchi

Watendaji wa kata na vijiji wilayani Handeni mkoani Tanga, wameonywa na kutakiwa kuacha kuwaruhusu wafuigaji kuingiza mifugo kwenye maeneo yao bila kufuata utaratibu. Atakaebainika kufanya hivyo atachukuliwa hatua za kisheria.

Onyo hilo limetolewa Novemba 18 na Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe, wakati akizindua zoezi la upigaji chapa mifugo (ng’ombe) wilayani humo katika kijiji cha Sua.

Gondwe amesema zipo taarifa kuwa kuna watendaji wa kata na vijiji bado wanapokea mifugo kinyemela.

Mkuu huyo wa wilaya alisema zoezi la kupiga chapa mifugo hiyo litasaidia kubaini mfugo katika kila eneo kutokana na alama zinazowekwa.

Alisema zipo taratibu za kupokea mifugo hivyo ni vizuri zifuatwe ili kuweza kuibaini mifugo ambayo inaweza kuingia na magonjwa na kusababisha maambukizi ya magonjwa.

Akielezea dhumuni ya zoezi hilo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, William Makufwe, alisema hikolo ni zoezi la kitaifa lililoagizwa kutoka ngazi za juu likiwa na nia ya kuondoa migogoro ya mara kwa mara, hivyo ni muhimu wafugaji wote kushiriki.

Alisema kwa halmashauri ya Handeni zaidi ya ng’ombe 30,000 wanatarajiwa kupigwa chapa ili iwe rahisi kutambuliwa, kuweza kusajiliwa na  kudhibiti mifugo iliyopo wilayani humo.

Aidha, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Handeni, Athumani Malunda, amewataka wafugaji kuepuka migogoro na wakulima kwa kulisha mifugo yao kwenye mashamba huku wakitoa lugha za maudhi  kwa wenzao.

Mmoja wa wafugaji mkazi wa Mkata, Omari Bigo, ameipongeza serikali  kwa kuendesha zoezi hilo na kusema kuwa litasaidia udhibiti wizi wa mifugo.

Serikali wilayani Handeni imetoa siku 45 hadi Disemba 31 kwa wafugaji wote kuhakikisha wamepeleka ng’ombe wao kupigwa chapa na atakayeshindwa kufanya hivyo atatozwa faini isiyozidi Sh1 milioni kwa kukiuka agizo.

-->