Ngeleja aibua maswali kibao

Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja akiwaonyesha waandishi wa habari, risiti ya malipo aliyoyafanya katika benki ya CRDB baada ya kurejesha serikalini sh40.4 milioni alizopewa na mmiliki wa Kampuni ya VIP Engineering and Marketing, James Rugemalira. Kulia ni Mkurugenzi msaidizi wa Idara ya Habari (Maelezo), Zamaradi Kawawa.Picha Said Khamis

Muktasari:

  • Ngeleja, ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, amechukua uamuzi huo takriban miaka mitatu baada ya Bunge kujadili kashfa hiyo na kutoa maazimio na siku chache baada ya watuhumiwa wawili katika sakata hilo kufikishwa mahakamani kwa makosa ya uhujumu uchumi.

Dar es Salaam. Kitendo cha mbunge wa Sengerema (CCM), William Ngeleja kurejesha serikalini Sh40.4 milioni zilizoingizwa kwenye akaunti yake, ikiwa ni sehemu ya fedha zilizochotwa kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow, kimeibua maswali tofauti.

Ngeleja, ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, amechukua uamuzi huo takriban miaka mitatu baada ya Bunge kujadili kashfa hiyo na kutoa maazimio na siku chache baada ya watuhumiwa wawili katika sakata hilo kufikishwa mahakamani kwa makosa ya uhujumu uchumi.

Tukio hilo pia limefanyika baada ya majaji wawili waliotajwa katika sakata hilo, Profesa Eudes Ruhangisa na Aloysius K. Mujulizi kuomba kustaafu kabla ya muda.

Kashfa hiyo, iliyoibuliwa na gazeti la The Citizen ambalo ni dada wa Mwananchi, ilihusisha Sh306 bilioni zilizowekwa Akaunti ya Tegeta Escrow iliyofunguliwa kwa pamoja na kampuni ya IPTL na Shirika la Umeme (Tanesco) kuhifadhi fedha za malipo wakati kampuni hizo mbili zikiwa katika mgogoro wa kimkataba.

Lakini, fedha hizo zilitolewa na baadhi zilionekana kuingizwa katika akaunti za viongozi wa dini, mawaziri, watumishi waandamizi wa Serikali na wanasiasa, akiwemo Ngeleja aliyevunja ukimya jana.

Ngeleja aliwaambia waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Maelezo jana kuwa licha ya kulipa kodi ya Sh13.14 milioni ambayo ni sawa na asilimia 30 ya Sh40.4 milioni alizopewa na mfanyabiashara James Rugemalira, ameona bora azirejeshe serikalini.

“Nilipokea msaada huu kama wapokeavyo wabunge wengine kwa nia njema bila ya kujua kuwa James Rugemalira angekuja kuhusishwa na kashfa ya fedha za akaunti ya escrow kama ilivyo sasa,” alisema Ngeleja ambaye alikuwepo bungeni wakati sakata la escrow lilipojadiliwa bungeni mwaka 2014.

“Kwa vile sasa imedhihirika kuwa aliyenipa msaada huu anatuhumiwa katika kashfa ya akaunti ya escrow, nimepima na kutafakari na hatimaye nimeamua kwa hiari yangu mwenyewe kurejesha serikalini (TRA) fedha zote nilizopewa kama msaada Sh40.4 milioni bila ya kujali kwamba nilishazilipia kodi ya mapato kama nilivyoeleza hapo awali. Risiti ya ushahidi wa kurejesha fedha hizi serikalini hii hapa.”

Alisema pamoja na ukweli kwamba aliyempa fedha hizo bado hajapatikana na hatia, ameamua kujitenga na tuhuma hizo kwa kuzirejesha.

Kuhusu kuchelewa kurudisha fedha hizo baada ya Rugemalira kutuhumiwa, Ngeleja alisema alishindwa kufanya hivyo mapema kwa kuwa haikuthibitishwa kama mfanyabiashara huyo ana kashfa.

Hadi sasa ni Rugemalira, ambaye anamiliki kampuni ya VIP Engineering iliyokuwa inamiliki asilimia 30 ya hisa za IPTL, na Harbinder Sing Sethi, mwenyekiti mtendaji wa Pan African Power Solution iliyoinunua kampuni hiyo ya ufuaji umeme, ndio pekee waliofikishwa mahakamani kuhusishwa na sakata hilo.

Akizungumza na Mwananchi Juni mwaka jana, mkurugenzi mkuu wa Takukuru, Valentino Mlowola alisema wote walioingiziwa fedha kutoka akaunti ya escrow watashughulikiwa kwa kuwa taasisi yake inaendelea kufuatilia sakata hilo.

“Yeyote aliyekula fedha hizo na kuna rekodi, asidhani kuwa (suala hilo) limeisha,” alisema Mlowola katika mahojiano maalumu na Mwananchi Juni mwaka jana.

Lakini kitendo cha Ngeleja kutangaza kurejesha fedha hizo jana, kinaibua maswali kama anataka kufuata nyayo za watuhumiwa wa sakata jingine la fedha zilizochotwa kutoka Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) walioitikia wito wa kurejesha fedha ili wasifikishwe mahakamani.

Katika sakata hilo la mwaka 2008, zaidi ya Sh133 bilioni zilichotwa na wafanyabiashara tofauti walioghushi nyaraka kudai wamerithishwa madeni na kampuni za nje.

Kitendo cha kurejesha fedha TRA badala ya Hazina pia kimeibua maswali mengine. Kazi ya TRA ni kukusanya kodi na tayari Ngeleja alishalipa Sh13.14 milioni, lakini jana alilipa Sh 40.4 kwenda kwa kamishna wa kodi za ndani TRA na kupewa risiti ya CRDB, benki aliyoitumia kutuma fedha hizo.

Mkurugenzi wa elimu kwa mlipa kodi na mawasiliano wa TRA, Richard Kayombo hakutaka kuzungumzia suala hilo, akisema Ngeleja ndio kwanza kalizungumzia na hivyo hawezi kusema lolote.

“Aulizwe mwenyewe, siwezi kucomment (kuzungumzia),” alisema Kayombo.

Pia, utata mwingine ni fedha hizo zimewekwa katika fungu gani baada ya kutumwa TRA. Kayombo alisisitiza hawezi kusema lolote.

Maswali mengine ni sababu ya kuhifadhi fedha hizo hadi leo wakati alikuwa ameziomba kama msaada kwa ajili ya wananchi wa jimboni kwake. Utata mwingine ni uwezo wake wakati akiomba fedha hizo na wakati huu ambao amezirejesha kama alishazitumia kwa shughuli za maendeleo ya jimboni kwake.

Kuna maswali mengi, lakini je kuzirejesha kutamfanya awe huru na vyombo vya dola?

Wengine waliopata mgawo

Mbali na Ngeleja, wengine waliopata mgawo huo ni Anna Tibaijuka, aliyekuwa Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Andrew Chenge (mbunge wa Bariadi Magharibi) ambao kila mmoja alipewa Sh1.6 bilioni.

Wengine ni Paul Kimiti (Sh40.4 milioni), Daniel Yona (Sh40.4 milioni), Dk Enos Bukuku (aliyekuwa mjumbe wa Bodi ya Tanesco), Jaji Ruhangisa (Sh404.25 milioni), Jaji Mujulizi (Sh40.4 milioni) na aliyekuwa mkurugenzi wa Mamlaka ya Usajili wa Vizazi na Vifo (Rita), Philip Saliboko (Sh40.4 milioni).

Pia, aliyekuwa mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), Emmanuel Daniel Ole Naiko (Sh40.4 milioni), Ofisa wa TRA, Lucy Appollo (Sh80.8 milioni), Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Methodius Kilaini (Sh80.9 milioni), Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Eusebius Nzigirwa (Sh40.4 milioni) na Padri Alphonce Twimannye Simon (Sh40.4 milioni).

Hatua hiyo ya Ngeleja imeungwa mkono na Askofu Kilaini ambaye amesema na yeye yuko tayari kuzirudisha.

Kauli kama hiyo ilitolewa na Ole Naiko aliyeiambia Mwananchi kuwa hakuwahi kutoa fedha hizo benki na wala hajashughulika na akaunti hiyo kwa kuwa hakuifungua.

Alisema hata iweje hatagusa hizo fedha kwa kuwa hajui zilikuwa zina mtego gani.

“Huwa sina utaratibu wa kuiangalia hiyo akaunti.”

Takukuru yazungumza

Kuhusu uwezekano wa kusamehewa vigogo watakaorejesha fedha za mgawo wa Escrow, msemaji wa Takukuru, Mussa Msalaba alisema suala hilo haliwezi kutolewa ufafanuzi kwa sasa kwa kuwa bado liko kwenye uchunguzi.

“Tunaendelea na uchunguzi wetu. Hatuwezi kusema sasa, kazi ni nyeti kwa hiyo inaweza kutuathiri,” alisema.

Sakata la IPTL, ambayo ina jenereta zinazotumia mafuta mazito kuzalisha umeme, na Tanesco lilitokana na kutokubaliana na kiwango cha tozo ya uwekezaji ambacho kampuni hiyo binafsi ilikuwa inaitoza Tanesco.

Baada ya kufikishana mahakamani, pande hizo mbili zilikubaliana kufungua akaunti ya escrow ili fedha hizo za malipo ziwe zinawekwa hadi baada ya uamuzi kutolewa.

Lakini wakati kukiwa na kesi tofauti, pande hizo mbili ziliridhia kutoa fedha hizo na kulipwa kampuni ya PAP iliyokuwa mmiliki mpya wa IPTL na baadaye kugawanywa kwa watu tofauti kupitia benki za Mkombozi na Stanbic. Hadi sasa waliolipwa kupitia Stanbic hawajajulikana.

Imeandikwa na Elizabeth Edward, Phinias Bashaya, Israel Mapunda na Kelvin Matandiko