Ngoma, vigodoro bado changamoto Mkuranga

Muktasari:

  • Imedaiwa kwamba baadhi ya wakazi wa Mkuranga wapo tayari kuchangia ngoma lakini kuhusu elimu hawatoi ushirikiano.
  • Watoto wamedaiwa kukimbia shule baada ya kujua mambo ya watu wazima wakiwa bado wadogo.
  • Wananchi wametakiwa kujua umuhimu wa elimu na kuacha kuwapoteza watoto ambao ni taifa la kesho

Mkuranga. Licha ya Serikali kuweka mkazo kwenye elimu kwa kuanzisha sera ya elimu bure ili watoto wote wapate fursa ya kupata elimu lengo hilo linaweza lisitimie mkoani Pwani kutokana na wakazi wa eneo kuendelea kutekeleza tamaduni hatarishi.

Tamaduni hizo ni pamoja na kuwacheza ngoma wasichana wadogo na kuwafundisha mambo ambayo yanawafanya wengi wao kukatiza masomo yao na kujiingiza kwenye mapenzi katika umri mdogo.

Hayo yamebainishwa na vijana wa kata mbalimbali za wilaya ya Mkuranga walipokutana katika warsha ya kujengewe uwezo, kujitambua na kushiriki katika uandaaji na utekelezaji wa sera zinazowahusu vijana iliyoandaliwa na asasi ya Social Information and Facilitation na kufadhiliwa na Foundation for Civil Society.

Takwimu zinaonyesha  wanafunzi 7151 walioandikishwa darasa la kwanza mwaka 2011 wakitarajiwa kuhitimu mwaka huu katika wilaya hiyo, lakini kati yao 963 wamekatisha  masomo yao.

Wakizungumza na Mwananchi vijana hao wamesema kwamba mila na desturi zimekuwa kichochezi kikubwa kwa wasichana wengi kukatisha masomo yao.

Mmoja wa vijana hao Tabia Mohamed amesema wasichana wengi ambao wamechezwa ngoma, huishia kufanya majaribio ya mafunzo waliyopewa unyagoni na matokeo yake huacha shule.

“Mwanafunzi anapopelekwa kwenye unyago akili yake inabadilika, ni wachache sana ambao wanaweza kurudisha mawazo yao darasani, wengi wanafikiria jinsi ya kuyafanyia kazi mafunzo waliyoyapata.

“Hapo ndipo unapokuta wengi wao wanakatisha masomo labda itokee kuna mzazi mwenye msimamo ndiyo anaweza kumlazimisha mwanae hadi amalize hilo darasa la saba,”

Kwa upande wake Ibrahim Ngaona alirusha  lawama kwa wazazi na jamii kwa ujumla kutokana na kukosa mwamko wa elimu na badala yake kuendekeza ngoma na sherehe.

“Yaani hapa kuna watoto wengine wanataka kusoma lakini hawana uwezo, mtu yuko radhi aweke ngoma wiki nzima nyumbani kwake, na watu wako tayari kuchangia lakini umwambie achangie elimu hakuna anayekubali kufanya hivyo,” amesema Ngaona

Ofisa maendeleo ya jamii wa wilaya hiyo Peter Nambunga amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo na athari zake huku akieleza kuwa serikali inaendelea kukabiliana nayo ili kumaliza kabisa.

Amesema tayari suala hilo limeshapelekwa kwenye baraza la madiwani ili litungiwe sheria ndogo ambazo zitawabana wazazi.

“Tumeliona hilo na sio hilo pekee kuna suala la vigodoro, kuonyesha video haya yote yanaleta changamoto ila tumeshawapelekea madiwani tunasubiri watunge sheria,” amesema Nambunga