Ngurumo ajibu kauli ya Serikali kuhusu kukimbia kwake nchini

Muktasari:

Juzi, Ngurumo alikaririwa na Mwananchi akisema ameamua kukimbilia Finland kutokana na kutishiwa maisha na kwamba waandishi wa habari nchini wapo hatarini akimtolea mfano mwandishi wa habari wa kujitegemea wa gazeti la Mwananchi, Azory Gwanda aliyetoweka tangu Novemba mwaka jana kwamba huenda ni kwa sababu kama za kwake.

Dar es Salaam. Siku moja baada ya Serikali kusema madai ya Ansbert Ngurumo kwamba alitishiwa maisha kwa kuikosoa na hivyo kukimbilia ughaibuni kuwa ni usanii na upuuzi, mwandishi huyo wa habari amesema majibu hayo yanaonyesha dharau.

Juzi, Ngurumo alikaririwa na Mwananchi akisema ameamua kukimbilia Finland kutokana na kutishiwa maisha na kwamba waandishi wa habari nchini wapo hatarini akimtolea mfano mwandishi wa habari wa kujitegemea wa gazeti la Mwananchi, Azory Gwanda aliyetoweka tangu Novemba mwaka jana kwamba huenda ni kwa sababu kama za kwake.

Lakini Msemaji wa Serikali, Dk Hassan Abbasi alijibu madai hayo akisema, “Ni upuuzi mtupu, kwa sababu anahusisha vitu visivyohusiana, kwani Azory katekwa na Serikali?”

Dk Abbasi ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari (Maelezo) alisema, “Ni usanii kwa sababu waandishi wa habari wanafanya shughuli zao vizuri na wanapokosea wanaambiwa na wanaikosoa Serikali vilevile.”

Jana, akizungumza kwa simu kutoka Finland, Ngurumo alisema Serikali haina rekodi nzuri juu ya watu wanaofuatilia na kuteka watu ndio maana haijui walipo Azory na Ben Saanane,ambaye ni msaidizi wa mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliyetoweka Novemba 2016.

“Wanaotenda maovu ya kuteka na kutesa watu ndani ya nchi na Serikali isijue ni kina nani? Kwa hiyo, kama vile wasivyowajua hao wasiojulikana, yawezekana hawajui suala langu pia,” alisema Ngurumo.

“Lakini kuna mtu mmoja hawezi kukataa hili, anajua, kwa kuwa alishiriki kuagiza niondolewe... anajua na anawajua vijana wawili aliowatuma Mwanza, tena wengine ni Wanyarwanda.”

Alisema kijana mmoja aliyetumwa kumfuatilia ni mkazi wa Lucherere Mwanza aliyemtaja kwa jina moja la Banny ambaye alidai kuwa ndiye aliyewapokea wengine na kuwapitisha katika hoteli na maeneo walikodhani wangemkuta.

“Kijana huyu Oktoba 10,2017 yeye ndiye aliyeenda kufanya upelelezi katika hoteli (anaitaja) iliyopo kona ya Bwiru baada ya kunikosa alienda hoteli ya (anaitaja), hakuona dalili lakini kuna watu walikuwa wakimfuatilia,” alidai Ngurumo.

Ngurumo alidai kwamba wasamaria wema ndiyo waliomsaidia kujificha na ndio waliokuwa wakiwafuatilia maadui waliokuwa wakimsaka katika miji ya Mwanza, Bukoba, Dar es Salaam na Biharamulo.

“Nina taarifa zao zote na hata magari waliyokuwa wanayatumia ni Toyota Prado, Toyota Harrier, Klugger.” alisema Ngurumo huku akitaja namba za usajili wa magari hayo na kuongeza:

“Atambue kuwa kuna watu wema ambao hawapendi matendo haya ya kikatili yanayofanywa na kikundi cha watu wachache.”

Ngurumo alisema katika kipindi chote cha kufuatiliwa na watu wasiojulikana hakuwahi kwenda kuripoti kituo chochote cha polisi juu ya suala hilo, “Niende polisi kujikamatisha? Si ningekuwa nimewasaidia kujua nilipo, sikwenda!” alisema Ngurumo.

Alisema mbali na kutoa taarifa kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter Oktoba 3, 2017 hakutaka tena kupiga kelele na badala yake aliendelea kupambana kimyakimya, kujilinda na kumulika wabaya wake akiwa mbali.

Alisema ni watu wachache waliofahamu shida alizokuwa anapitia na hakutaka kuweka wazi kwa kile alichodai kuwa miongoni mwa wabaya wake, baadhi yao ni watu wake wa karibu.

“Nina taarifa zao nyingi na mpaka sasa wanasikitika kwa nini niliwatoroka licha ya kuwa agizo lilitolewa nipelekwe nikiwa mfu,” alidai.

Kuhusiana na suala la ubalozi wa Finland nchini Tanzania kuwa na taarifa zake, Ngurumo alisema “ Wengine hata hayawahusu kabisa, wanaohusika ni idara ya Uhamiaji ya Finland huku niliko ndiyo wana taarifa zangu.”