Ngurumo aomba hifadhi Finland, Serikali yasema ni usanii, upuuzi

Muktasari:

Taarifa za Ngurumo za kuikimbia nchi na kuomba ulinzi wa kimataifa Finland zimepatikana katika makala iliyochapishwa kwenye tovuti ya taasisi isiyo ya kiserikali ya Kepa ya Finland, ambako ametambulishwa kama mwandishi mwalikwa wa makala za uchambuzi katika tovuti hiyo.

Wakati mwandishi wa habari nchini, Ansbert Ngurumo akidai kuwa ameamua kuomba hifadhi ya kimataifa nchini Finland baada ya kutishiwa maisha, Serikali imesema madai ya Ngurumo ni usanii na hayana mashiko.

Taarifa za Ngurumo za kuikimbia nchi na kuomba ulinzi wa kimataifa Finland zimepatikana katika makala iliyochapishwa kwenye tovuti ya taasisi isiyo ya kiserikali ya Kepa ya Finland, ambako ametambulishwa kama mwandishi mwalikwa wa makala za uchambuzi katika tovuti hiyo.

Katika makala hiyo, Ngurumo amesema alipata vitisho vya kuuawa kutoka kwa watu aliodai ni wa Serikali baada ya kuikosoa mamlaka ya juu.

Hata hivyo, Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbas akizungumza na Mwananchi jana alisema hoja ya Ngurumo kutishiwa maisha kwa kuikosoa Serikali si ya kweli kwani waandishi wa habari nchini wanafanya shughuli zao na wanapokosea wanaambiwa.

“Ni usanii, kwa sababu waandishi wa habari wanafanya shughuli zao vizuri na wanapokosea wanaambiwa na wanaikosoa Serikali vilevile,” alisema mkurugenzi mkuu wa Idara ya Habari (Maelezo).

Lakini, Ngurumo katika maelezo yake anasema waandishi wapo hatarini nchini na kumtolea mfano mwandishi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Azory Gwanda kuwa ametoweka tangu Novemba mwaka jana pengine kwa sababu kama zinazofanana na za kwake.

Hata hivyo Abbas alijibu kuwa Ngurumo anafananisha vitu visivyohusiana.

“Ni upuuzi mtupu, kwa sababu anahusisha vitu visivyohusiana, kwani Azory katekwa na Serikali?” alihoji

Ngurumo alisema alianza kuonywa Oktoba mwaka jana na wasamaria wema kuhusu kuwepo kwa mpango wa kumuua kwa kile alichodai amekuwa akiikosoa mamlaka ya juu.

Ngurumo alikuwa ni mhariri na mchambuzi wa gazeti la Mwanahalisi ambalo limefungiwa kwa miaka miwili tangu Septemba mwaka jana.

“Wakati Azory anatoweka Novemba mwaka jana, mimi tayari nilikuwa nimesaidiwa na kuhamishiwa Kenya, naishukuru Taasisi ya Kuwalinda Wanahabari ya Kenya,(CPJ) yenye makao makuu yake New York, Marekani,”

Aliongeza, “Lazima ziwepo jitihada za kuwalinda wanahabari, wasanii, wanasiasa na wanaharakati ambao hupata vitisho kutokana na kazi zao.”

Alisimulia kuwa wakati yupo katika vitisho hivyo vya kuuawa, aliwahi kuhama hoteli nne kwa usiku mmoja.

Kwa maelezo ya Ngurumo, katika moja ya hoteli alizolala, mkurugenzi wa hoteli alimwambia aondoke kwa kuwa amedokezwa na watu kuwa ‘wanaomtafuta’ wamejua alipo na wamemuhoji.

“Ni wiki mbili za shida, nikihama kutoka eneo moja kwenda jingine, nchi moja kwenda nyingine ili kutafuta hifadhi,” alisema.

Alisema alisafiri na kwenda kwa rafiki yake, mwanahabari ambaye pia ni mwakilishi wa Chadema ambaye alimsaidia kupata malazi kwa usiku huo na baada ya siku kadhaa alikwenda Nairobi.

“Nilipata hifadhi katika chumba cha taasisi inayofanya kazi na wajane na yatima. Nikagundua kuwa leo hii mimi baba wa watoto watano, sasa nilikuwa nasaidiwa na yatima na wajane,” alisema.

Akizungumza na Mwananchi jana, mbunge wa Jimbo la Ubungo Saed Kubenea alisema hata yeye taarifa za Ngurumo kupewa hifadhi Finland amezisoma katika mitandao ya kijamii na hakuwahi kuongea naye chochote.

“Aliwahi kuniambia kuwa maisha yake yapo hatarini kutokana na kutafutwa na watu wasiojulikana, wanafuatilia nyendo zake na hata waliwahi kumfuata Mwanza nyumbani kwake hadi ilifikia wakati akawa analala ofisini,” alisema Kubenea, ambaye ni mmiliki wa gazeti lililofungiwa la Mwanahalisi.

Kubenea alisema hiyo ilitokana na makala yake aliyowahi kuiandika katika gazeti la Mwanahalisi ambayo ilisababisha gazeti kufungiwa kwa miaka miwili.

“Mimi ninavyofahamu kuna muda alikuwa Nairobi wakati Tundu Lissu amelazwa nikadhani alienda kumuona na katika wale watu waliochaguliwa kumsindikiza na yeye alikuwepo labda baada ya kwenda huko alienda Sweden ndiyo akafika mpaka Finland aliko sasa,” alisema Kubenea.

Msemaji wa Jeshi la Polisi, Barnabas Mwakalukwa alipotafutwa kueleza iwapo ana taarifa za Ngurumo kutishiwa maisha, alisema hawezi kuzungumza kwa kuwa yupo nje ya mkoa.

Juhudi za kuupata ubalozi wa Finland Tanzania, hazikuzaa matunda.

UTILITI

Unapataje hifadhi katika nchi nyingine?

Mtaalamu wa masuala ya siasa na Diplomasia,Dk Benard Achiula kutoka Chuo cha Taifa cha Diplomasia anafafanua.

*Mtu anaweza kupata hifadhi kwenye nchi nyingine ikiwa amekumbwa na misukosuko ya kisiasa au kidini kwenye nchi yake.

*Kwa mfano Ujerumani imeweka Sheria inayompa kinga mtu yeyote aliyenyanyaswa kisiasa au kidini lakini kila nchi ina utaratibu wake.

*Ili mtu apate hifadhi nchi nyingine ni lazima afuate taratibu zilizowekwa ikiwamo kupata kibali na Serikali ya nchi husika.

*Ukifika pale unawekwa kwenye makambi halafu wanachunguza madai yako kama ni ya kweli kama unavyojua wahamiaji wengi wanasingizia kuteswa kisiasa japo wengi wao wana matatizo ya kiuchumi

*Mara baada Serikali kujiridhisha na madai unapewa kibali kinachokutambulisha kama mkimbizi aliyekubalika.

*Ukikubalika unapata kibali na hapo unaweza kufanya kazi kama mkimbizi aliyekubalika na endapo hutakubailiwa unaweza kudai haki mahakamani.