Ni kwa nini Kofi Annan aendelee kukumbukwa?

Muktasari:

  • Licha ya kufariki dunia kwa kiongozi huyo bado atakumbukwa alivyojitoa kutatua masuala ya kisiasa barani Afrika

Vizuri huwa havidumu hivi ndivyo unavyoweza kusema baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) kupoteza uhai ghafla akiwa hospitalini mbele ya familia yake.

Annan kwa miaka 10 mfululizo alikuwa kwenye kilele cha siasa za ulimwengu.

Aliendelea kufanya kazi kama balozi wa amani hata baada ya kuondoka kwenye nafasi ya ukatibu mkuu wa Umoja huo.

Baba yake alikuwa gavana wa jimbo la Ashanti chini ya utawala wa kikoloni wa Waingereza. Annan alisoma shule za kifahari Ghana, Uswisi na baadaye Marekani.

Annan alijiunga na UN akiwa na umri wa miaka 24, kama msimamizi katika Shirika la Afya Duniani (WHO) kisha akawa mkuu wa watumishi wa ujumbe wa UN mji mkuu wa Misri, Cairo.

Baada ya hapo alipata nafasi ya Naibu Mkurugenzi wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR ) Geneva, Uswisi na hatimaye akawa mkuu wa operesheni za kulinda amani mwaka 1993.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa wakati huo, Boutros Boutros-Ghali alimteua Annan kuwa naibu katibu mkuu katika masuala ya kulinda amani, alisimamia jeshi la kulinda amani la UN lililokuwa na askari 75,000 duniani kote.

Kama mkuu wa askari wa ulinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa, Annan alipata msukosuko akiwa kazini mwaka 1994 wakati wanamgambo wa Kihutu wenye msimamo uliokithiri walipowaua zaidi ya Watutsi 800,000 na Wahutu waliokuwa na msimamo wa wastani. Baadaye mauaji hayo yalitajwa kama mauaji ya kimbari ya Rwanda.

Annan alilaumiwa kwa kushindwa kutoa msaada wa kutosha katika nchi hiyo ya mashariki mwa Afrika licha ya onyo la awali juu ya kuongezeka kwa ukatili lililotolewa na Romeo Dallaire, mkuu wa jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa nchini Rwanda.

Kusita kwake kulitokana na ukweli kwamba Marekani na Ulaya zilionekana kuwa na masilahi madogo ya kujihusisha au kushiriki katika masuala ya Rwanda.

Annan aliomba radhi kwa niaba ya UN miaka 10 baadaye kwa kusema: “Jumuiya ya kimataifa imeshindwa kuinusuru Rwanda, hiyo inatupasa daima kuwa na hisia za majuto, uchungu na huzuni ya kudumu.”

Hakuwahi kukata tamaa

Alichaguliwa kuwa katibu mkuu Desemba 1997, baada ya Marekani kushinikiza, hivyo akawa Mwafrika wa kwanza kutoka eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara kuchukua nafasi hiyo.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, alieleza kuwa hakutaka kufanya kazi za utawala kama mkuu wa UN lakini pia alitaka kuunda upya siasa za kimataifa.

Ajenda yake ilikuwa ni pamoja na kupambana na umaskini wa kimataifa, kiwango cha kuongezeka joto duniani, Ukimwi na pia ufumbuzi wa migogoro ya kisiasa.

Baadaye, alieleza kuhusu kusainiwa kwa Malengo ya Maendeleo ya Milenia ya mwaka 2000 kuwa ni kielelezo kikuu cha kipindi chake katika ofisi.

Annan pia, alisimama kama mwakilishi katika mgogoro wa Cyprus na Iran juu ya mpango wake wa nyuklia. Alikuwa mkosoaji mkubwa wa mashambulizi yaliyofanywa na wanamgambo wa Sudan Janjaweed katika jimbo la Darfur.

Mwaka 2001, kamati ya tuzo ya kimataifa ya Amani ya Nobel ya Norway iliitambua michango ya Annan, na kumtunukia yeye na Umoja wa Mataifa kwa Tuzo ya Amani ya Nobel.

Mwenyekiti wa jopo la Oslo, Gunnar Berge, aliliambia Shirika la Habari la DW katika mahojiano kwamba Annan alikuwa mwakilishi bora wa UN na katibu mkuu aliyefanya kazi kwa ufanisi katika historia ya Umoja wa Mataifa.

Ilichosema familia

Familia ya Annan imesema kwamba ndugu yao huyo alipoteza maisha kwa amani baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Taarifa ya familia hiyo ilisema kwamba Annan alifariki dunia kwa amani Jumamosi baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Katibu Mkuu aliyepita Ban Ki-moon, alisema Annan aliweza kuiongoza UN katika karne ya 21 akielekeza ajenda muhimu ambazo ziliufanya Umoja huo kuwa na mwelekeo halisi wa amani, ufanisi na heshima ya utu duniani kote.

Annan alifariki dunia akiwa hospitalini katika eneo linalozungumza Kijerumani la nchi hiyo, shirika la habari la Uswisi ATS, limeripoti.

Katibu Mkuu wa sasa Antonio Guterres alimueleza mtangulizi wake huyo kuwa, ni nguvu inayoelekeza kwa ajili ya mambo mema.

Alisema Annan alipanda kupitia ngazi mbalimbali na kuliongoza shirika hilo katika milenia mpya kwa heshima ambayo haina mfano na dhamira.

Umoja wa Mataifa ulitoa taarifa kwamba bendera itapeperushwa nusu mlingoti katika maeneo yake yote duniani kote kesho.

Pia Rais wa Ghana, Nana Akufo- Addo alitangaza wiki ya maombolezo kwa kumkumbuka kiongozi huyo aliyeliletea Taifa hilo sifa.

Mwaka 2001, wakati dunia ikiwa katika mtafaruku wa shambulio la kigaidi la Septemba 11 nchini Marekani, Annan alipewa tuzo ya amani ya Nobel kwa pamoja na taasisi hiyo ya dunia kwa kazi yake ya kuiweka dunia kwenye amani.

Mshindi mwingine wa tuzo ya amani ya Nobel, askofu mstaafu Desmond Tutu, alimueleza Annan kuwa ni binadamu maarufu ambaye ameliwakilisha bara la Afrika na dunia kwa neema, heshima na nidhamu.

Annan aliyezaliwa mjini Kumasi, mji mkuu wa jimbo la Ashanti nchini Ghana, alifanyakazi kwa miongo minne akiwa UN. Pia, alikuwa mkuu wa kwanza wa taasisi hiyo akitokea katika shirika hilo.

Kutoka katika Bara la Afrika hadi Marekani, salamu za maombolezi zilimiminika kutoka kwa viongozi duniani kote jana Jumapili, baada ya Annan kufariki dunia.

Kiongozi huyo wa UN na mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel, na mwanadiplomasia nyota, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 80.

Raia huyo wa Ghana alikuwa mwanadiplomasia ambaye alipata sifa sehemu kubwa kwa kupandisha hadhi ya taasisi hiyo katika siasa za dunia wakati wa vipindi viwili akiwa mkuu kuanzia mwaka 1997 hadi 2006.

Pia, aliuongoza umoja huo katika miaka ya mtengano katika vita vya Iraq na baadaye alishutumiwa kwa rushwa katika kashfa ya mafuta na chakula, moja kati ya nyakati ngumu kabisa katika kipindi chake cha uongozi.

Alichokifanya Kenya

Annan ambaye alikuwa mpatanishi mkuu baada ya mgogoro wa kisiasa Kenya miaka kumi iliyopita, alitoa wito kwa walioshindwa kutumia mifumo ya kisheria kutafuta haki.

Alikuwa mpatanishi mkuu baada ya ghasia kuzuka katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2007 uliokumbwa na utata.

Mwai Kibaki alitangazwa mshindi wakati huo lakini Raila Odinga na chama chake cha ODM wakapinga matokeo hayo.

Katibu mkuu huyo wa zamani wa UN alimpongeza Kenyatta kwa ushindi wake na pia akamsifu Odinga kwa kuendesha kampeni yake kwa njia ya amani.

“Namshukuru kiongozi wa upinzani Raila Odinga kwa kampeni ya uchaguzi ya amani aliyoiendesha. Amekuwa mtetezi jasiri wa demokrasia,” alisema Annan kupitia taarifa.

“Kwa hivyo, namhimiza sasa afuatilie malalamiko yake kupitia mifumo ya kisheria iliyowekwa na aweke masilahi ya taifa mbele, kama alivyofanya kwa uzalendo mara nyingi awali.”

Upinzani umekuwa ukidai mitambo ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (IEBC) ilidukuliwa na matokeo kuchakachuliwa kumsaidia Rais Kenyatta.

Rais Kenyatta alipata kura 8, 203, 290 ambayo ni asilimia 54.27 naye mpinzani wake mkuu, mgombea wa muungano wa upinzani wa National Super Alliance Raila Odinga akapata kura milioni 6,762,224 ambayo ni asilimia 44.74.