Ni kweli, vita dawa za kulevya inyooshwe

Muktasari:

Katika habari hiyo, Ridhiwan anaeleza jinsi alivyoitwa na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya, Rogers Sianga na kuhojiwa kuhusu tuhuma dhidi yake kuwa anajihusisha na biashara ya dawa hizo haramu

Katika toleo letu la jana ukurasa wa tatu kulikuwa na habari inayomuhusu mbunge wa Chalinze (CCM), Ridhiwan Kikwete ikizungumzia operesheni inayoendelea ya kupambana na dawa za kulevya.

Katika habari hiyo, Ridhiwan anaeleza jinsi alivyoitwa na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya, Rogers Sianga na kuhojiwa kuhusu tuhuma dhidi yake kuwa anajihusisha na biashara ya dawa hizo haramu.

Mwishoni mwa habari hiyo, mtoto huyo wa Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne anaeleza maoni yake kuhusu mchakato mzima wa kusaka watu wanaojihusisha kuuza au kutumia dawa hizo.

Kwa mujibu wa Ridhiwan, ni muhimu kwa Serikali kuweka bayana ni chombo gani hasa kinatakiwa kiendeshe vita hiyo badala ya hali iliyopo sasa ambayo Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya inahoji watuhumiwa, huku Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam nalo likiendesha operesheni yake.

Ni kitu ambacho hakipingiki kwamba kila Mtanzania, kila taasisi na kila mtu anafaa kushiriki katika vita hiyo, lakini kila anayeshiriki ni lazima ashiriki kwa nafasi yake na kwa mujibu wa taratibu zilizopo.

Ridhiwan anasema kuwa wakati Sianga akitumia orodha ya watu 96 aliyokabidhiwa, kuita watu na kuwahoji bila ya kuwabugudhi, kamanda wa Jeshi la Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro anatumia mbinu tofauti.

Anatangaza majina ya watu anaotaka kuwahoji na kuwaita polisi. Na haishii hapo; baadhi anawaweka ndani kwa siku kadhaa kabla ya kuwaachia.

Hii inasababisha kuwepo kwa maneno ambayo hayana ulazima. Kwamba baadhi ya watu wanaitwa kimyakimya na kuhojiwa na wengine wanatangazwa, kuhojiwa na kuwekwa ndani bila ya kuelezwa kwa kina sababu za watuhumiwa wawili wa kosa moja kushughulikiwa kwa njia tofauti.

Kama Ridhiwan alivyosema ni muhimu vita hii ikajengewa misingi ili isitumike vibaya au kutafsiriwa vibaya na wananchi. Jeshi la Polisi lina mamlaka yake katika vita yoyote dhidi ya uovu katika jamii.

Lakini kwa sababu Rais ameshateua watu ambao wanatakiwa kuongoza Mamlaka ya Kupambana na dawa za Kulevya, Jeshi la Polisi halina budi sasa kufanya kazi kwa maagizo ya chombo hicho ili kusiwepo na muingiliano wa majukumu ambayo yanaweza kuvuruga hata nia njema ya kupambana na dawa hizo.

Tunajua mamlaka imeshawekewa taratibu zake za kupambana na dawa hizo na pia imeshainishiwa jinsi itakavyoshirikiana na vyombo vingine vinavyofanya kazi hiyo hiyo kwa njia nyingine kama kukamata na kupima, hivyo kila chombo kibakie katika majukumu yake ya kisheria.

Pamoja na Jeshi la Polisi, wanasiasa pia waiachie mamlaka ifanye kazi yake. Wanasiasa ambao wanapata taarifa za kuwepo kwa watu wanaojihusisha na uuzaji au utumiaji wa dawa hizo kupitia kamati zao za ulinzi na usalama, hawana budi sasa kushirikiana na Mamlaka hiyo kuona ni jinsi gani watuhumiwa wanaweza kukamatwa na hatimaye kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Kuwa na uchungu na nchi dhidi ya watu wanaofanya biashara inayoharibu kizazi kijacho, kunatakiwa kuendane na taratibu zilizopo za kuwashughulikia watuhumiwa kwa kuwa tayari sheria ipo na chombo kilichokabidhiwa jukumu hilo kisheria kimeshaundwa.

Sisi wote-wananchi wa kawaida, viongozi wa Serikali, Jeshi la Polisi na wanasiasa- tunatakiwa kuisaidia Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya kufanya kazi yake kwa ufanisi kwa kuipa taarifa zote muhimu badala ya sisi kuzifanyia kazi kwa kuwasaka watu wanaotajwa kuhusika na matumizi na biashara ya dawa za kulevya.