Ni kweli dalili hizi kwa mjamzito zinatafsiri jinsi ya mtoto?

Muktasari:

Nina imani mama yangu ni mmoja wa wanawake walio wengi na kama si karibu wote ambao kwa muda wote wa uja uzito huwa hawajui jinsi ya mtoto aliyembeba tumboni hadi siku ya kujifungua.

Mama yangu mzazi aliwahi kuniambia hakuwahi kuijua jinsi yangu kwa muda wote wa ujauzito hadi siku niliyozaliwa.

Nina imani mama yangu ni mmoja wa wanawake walio wengi na kama si karibu wote ambao kwa muda wote wa uja uzito huwa hawajui jinsi ya mtoto aliyembeba tumboni hadi siku ya kujifungua.

Hii haijawahahi kuwa ajabu na hasa kwa miaka ya nyuma ambayo sayansi na teknolojia ilikuwa bado ya kiwango cha chini, lakini habari njema ni kwamba, sasa hivi wanawake wanaweza kufanyiwa vipimo na kugundulika jinsi za watoto wao wangali bado wakiwa tumboni kama itahitajika kufanya hivyo.

Japo pia huduma hizi hazijafanikiwa kuwafikia wanawake wote na hasa wale waishio vivijini kutokana na uhaba wa vifaa vya radiolojia kama vile mashine za “ultrasound” ambazo ndizo zinazotumika kugundua jinsi ya mtoto akiwa tumboni.

Lakini pia bado nimeona kuna baadhi ya wanawake huchagua kutojua jinsi ya mtoto hadi siku atakayojifungua kwa dhana kwamba, jinsi ya mtoto ni “surprise” kutoka kwa Mungu mwenyewe.

Lakini pamoja na haya yote, kama inavyofahamika, tangu siku ya kwanza mwanamke anapojigundua ni mjamzito hadi siku ya mwisho anapojifungua, hupita safari ya miezi tisa iliyochanganyika na mabadiliko mengi.

Mabadiliko haya huja kwa sura tofauti na kugusa mifumo karibu yote kwenye mwili wake na hasa kisaikolojia, kwenye mfumo wa chakula, mfumo wa vichocheo, na mfumo wa uzazi na uzazi wenyewe kutokana na maendeleo ya ukuaji wa mtoto awapo tumboni.

Mabadiliko haya yanapotokea, husababisha pia dalili mbalimbali zinazojitokeza mwilini na kupitia dalili hizi, wanawake wenyewe huzitumia kama ishara za kutafsiri jinsi ya mtoto kama ni wa kike au wa kiume kulingana na dalili husika ambayo mjamzito mwenyewe huipitia.

Inasemekana kwa miaka iliyopita zimekuwa dhahiri na hata sasa baadhi ya wanawake wanazisadiki na kukiri kuwa ni kweli dalili hizi zinatafsiri jinsi ya mtoto.

Lakini je, hii imekaaje kisayansi?

Dalili ya kwanza ni uchovu mkali wakati wa asubuhi. Wajawazito zaidi ya sita kati ya 10 hupitia tatizo la uchovu mkali asubuhi baada ya kuamka hasa kwa miezi mitatu ya kwanza.

Wengi wao husadiki kuwa hali hiyo mara nyingi huashiria mtoto atakayezaliwa ni wa kike. Kisayansi ipo hivi, mwanamke mwenye ujauzito wa mtoto wa kike anakuwa na kiwango kikubwa cha vichocheo na humsababishia uchovu mkubwa, lakini mjamzito mwenye mtoto wa kiume hubeba kiwango kidogo cha homoni au vichocheo na hivyo kumfanya awe na uchovu wa kawaida hasa wakati wa asubuhi.

Dalili nyingine kubwa ni mihemko ya hisia. Kuna baadhi ya wajawazito wanakuwa na tabia za kubadilika na huwa wepesi wa kukasirika bila sababu ya msingi.

Watu wengi hudhani wajawazito wa namna hii watajifungua watoto wa kiume na wale ambao wanakuwa si wa kubadilika badilika, watajifungua watoto wa kike.

Lakini ukweli ni kwamba, wajawazito wote hupitia hali ya mabadiliko ya mihemko hasa muhula wa kwanza na wa tatu wa ujauzito.

Na pia, kubadilika kwa mihemko kunachangiwa na mambo mengi ikiwamo msongo wa mawazo, vichocheo na sababu zingine za kisaiokolojia, hivyo dalili hii haina uhusiano na jinsi ya mtoto.