Ni zamu ya Dk Kigwangalla bungeni leo

Muktasari:

  • Wiki iliyopita ilishuhudiwa Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba na wa Mifugo na Uvuvi, Luhanga Mpina wakipata wakati mgumu kutoka kwa wabunge kutokana kubanwa baada ya kushindwa kuwapa majibu ya kuridhisha ya hoja zao.

Dodoma. Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla leo atawasilisha bungeni hotuba ya bajeti ya wizara kwa mwaka wa fedha 2018/19.

Wiki iliyopita ilishuhudiwa Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba na wa Mifugo na Uvuvi, Luhanga Mpina wakipata wakati mgumu kutoka kwa wabunge kutokana kubanwa baada ya kushindwa kuwapa majibu ya kuridhisha ya hoja zao.

Wakati hayo yakitokea kwa mawaziri hao, bajeti ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa iliyowasilishwa na waziri Dk Hussein Mwinyi ilipita kirahisi ikiungwa mkono na wabunge wengi.

Dk Kigwangalla na naibu wake, Japhet Hasunga kwa siku mbili leo na kesho, watalazimika kusikiliza kwa makini na kuandaa majibu ya hoja za wabunge.

Kuwasilishwa kwa bajeti hiyo kutafanya idadi ya wizara zilizosalia kuwasilisha hotuba zake kuwa tano ambazo ni Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa; Nishati; Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Madini; na Fedha na Mipango kabla ya kusomwa bajeti kuu ya Serikali Juni 14 saa 10:00 jioni.

Akizungumza na mwandishi wetu jana, msemaji wa kambi rasmi ya upinzani bungeni kwa wizara ya Maliasili na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa alisema licha ya wizara hiyo kupata waziri kijana bado haijaonyesha tofauti.

“Sitarajii kitu kikubwa katika bajeti ya Kigwangalla, kuna mambo mengi yametokea tangu aingie wizarani hapo, hakutaka kujifunza kutoka kwa waliomtangulia, jambo ambalo limeendelea kuathiri utalii na kuikosesha Serikali mapato,” alisema.

Mchungaji Msigwa alisema, “Kuna vitalu 81 havina wawekezaji, kitendo hicho kinaikosesha mapato nchi, alitakiwa kujifunza kipi cha kufanya lakini anafanya mambo anavyojua na ni matarajio yangu kama ilivyokuwa kwa bajeti nyingine, hii nayo itakuwa na mtikisiko.”

Mchungaji Msigwa ambaye ni mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), alisema umefika wakati kwa waziri anayeongoza wizara hiyo kusafiri nje ya nchi kutangaza utalii na kuhudhuria makongamano ya kimataifa badala ya kuutangaza akiwa nchini.

Mbunge wa Buhigwe (CCM), Albert Obama alitofautiana na Mchungaji Msigwa akisema, “Sitarajii kama kutakuwa na mvutano, itakwenda vizuri tu.”

Obama alisema tatizo linaloikumba wizara hiyo ni migogoro kati ya hifadhi na wananchi na fidia kwa wanaoumizwa na wanyama; maeneo aliyosema yanapaswa kuangaliwa na wizara.