Nilikuwa na zaidi ya milioni harusini kwa Shilole

Muktasari:

Kuoa ni jambo jema hata kwa Mwenyezi Mungu

Mwanamuziki Dogo Janja amesema wakati anamtunza msanii Zuwena Mohamed, kwenye harusi yake alikuwa na kitita cha zaidi ya Sh1 milioni mkononi.

Akizungumza na Mwananchi, Dogo Janja alisema ilipofika muda wa kuwatunza maharusi alichojua ni kufungua tu rubber band na hakumbiki ni kiasi gani alichotoa kwa kuwa yeye sio mtu wakuhesabu hela mara kwa mara.

“Unajua ni kawaida yangu kutembea na fedha nyingi mfukoni, na hata nikiwa kwenye harusi ya dada yangu Shilole na ndugu yangu Uchebe nilikuwa nina zaidi ya milioni mfukoni na wala sikumbuki ukumbini pale niliacha kiasi gani ila ilikuwa fedha nyingi,” amesema.

Akizungumzia sababu iliyomfanya kutoa fedha zote hizo, msanii huyu amesema ni kutokana na kufurahishwa na mwanaume mwenzake Uchebe kuingia katika kundi la watu wanaoruhusiwa kula kombe kama alivyofanya yeye siku za karibuni kwa kumuoa Irene Uwoya.

Alisema kuoa ni jambo jema hata kwa Mwenyezi Mungu ukizingatia na maisha ya ujana ambayo yamewazunguka watu wenye umri kama yeye, hivyo alikuwa na kila sababu ya kufurahi na kuwaunga maharusi hao mkono.