Steve Nyerere: Nimeacha ‘kiherehere’ kwenye misiba ya wasanii

Steve Nyerere


Muktasari:

Steven anasema anachoona ni kuwa kunatakiwa kuzalishwa wasanii wapya

Steve Nyerere ni kati ya wasanii wenye majina makubwa hapa Bongo, na jina lake lilipata umaarufu kutokana na kuigiza sauti za viongozi mbalimbali.

Moja ya sauti zilizompa umaarufu ni ile ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na ndio iliyompa jina hilo la Steve Nyerere, ambapo baadaye aliamua kuingia kwenye tasnia ya filamu huku ya kwanza kuitoa ilikwenda kwa jina la My Son.

Steve ambaye jina lake halisi ni Steven Mengele, pia amejizolea umaarufu kutokana na namna alivyoweza kuwaunganisha wasanii waliokuwa klabu ya Bongo Movie kwa yeye kuwa katibu.

Pia amekuwa mmoja wa wasanii wanaojitolea kusimamimia shughuli mbalimbali za wasanii ikiwemo misiba na nyinginezo.

Pamoja na nia yake hiyo nzuri kumekuwapo na maneno yanayosemwa juu yake hususan katika mitandao ya kijamii ya kuwa msemaji katika kila misiba.

Maneno hayo yamelifanya gazeti la Mwananchi kumtafuta ili kujua nini hasa siri ya yeye kuwa hivyo na kama hayo maneno yameshamfikia anayaongeleaje.

Katika maelezo yake, Steve anasema watu wanapaswa kuelewa kwamba anaposimamia shughuli mbalimbali za misiba si kwamba yeye ndiye ametaka, ila ni watu wanampendekeza.

“Kwangu hili naliona ni jambo jema, kwani mpaka watu wanakuchagua mtu fulani kusimamia jambo fulani ni wazi kwamba wanakuamini.

‘Japokuwa nasikitika pamoja na juhudi zote ninazozifanya na kuhakikisha shughuli hizo ninazopewa majukumu zinaenda vizuri hadi mwisho, naambulia matusi na lawama, tena lawama zenyewe nyingi zinatoka kwa wasanii wenzangu,” anasema.

Kutokana na kuchoshwa huko, Steve ambaye alishawahi kutaka kugombea ubunge zaidi ya mara tatu katika Jimbo la Kinondoni kupitia tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na kupigwa chini katika hatua za kura za maoni, anasema kuanzia sasa atabaki kuwa muombolezaji kama watu wengine, kwani maneno yanayosemwa dhidi yake hayamuumizi tu yeye tu bali familia na marafiki zake.

Anasema anasikitika wakati alipokuwa akifanya shughuli hizo, kazi zake nyingine zilikuwa zikilala na alikuwa akifanya kwa mapenzi ya kuwa kioo cha kuwaunganisha wasanii wengine, hivyo alichoamua sasa ni kujikita zaidi katika kazi zake ikiwemo kuendeleza kampeni yake ya uzalendo kwanza.

“Katika kampeni ya uzalendo kwanza nina kazi nyingi za kufanya mpaka sijui nianze na ipi niache ipi, na ninashukuru hivi sasa Watanzania wameanza kuingiwa na uzalendo tofauti na ilivyokuwa hapo nyuma, hivyo ngoja nijikite huko zaidi ili vizazi vijavyo huenda vikaja kukumbuka mchango wangu kuliko hizi kazi zisizoisha lawama za misiba,”anasema.

Bongo Movie

Kuhusu Bongo Movie, Steven anasema anachoona ni kuwa kunatakiwa kuzalishwa wasanii wapya ndani ya klabu hiyo, kwa kuwa waliopo wengi ni wanafiki na wachoyo.

Anasema imefika mahala ndani ya klabu hiyo, msanii na msanii wanatukanana jambo ambalo ni nadra kwa wasanii wa nchi nyingine kama Nollywood na Hollywood kulikuta katika umoja wao. “Ifike mahali wasanii waheshimiane kuanzia kwenye maisha ya kawaida hadi kwenye kazi zetu, ambapo wengi waliongia huko hawakuchukulia kama kazi ya filamu ni ajira katika maisha yao na badala yake waliona kama ni uchochoro wa kupatia umaarufu.

“Lakini naomba niwahakikishie kwamba klabu ya Bongo Movie katu haiwezi kufa bali wasanii wasiokuwa na vigezo ndio watakaondoka mmoja baada ya mwingine na watazaliwa wapya,” anasema.

Kuigiza vipi?

Akizungumzia kuendelea kuigiza, anasema kwa sasa amesimama akiangalia soko na kwamba hawezi kutengeneza kazi ya Sh30 milioni akaambulia milioni tatu, kwa kuwa ndio soko la filamu lilipokuwa limefika.

Hivyo anachosubiri ni kushughulika na kazi zake nyingine mpaka hapo sanaa hiyo itakapokaa sawa huku akieleza kuwa tayari wameshamfikishia kilio chao Rais Magufuli cha kuhakikisha anabadilisha baadhi ya mambo katika tasnia hiyo, ikiwemo suala la kutouza hatimiliki na liwekwe hadi kwenye Katiba ya nchi.

Pia anasema ili filamu za Tanzania ziwe nzuri ni vyema wasanii wakaachiwa uhuru wa kuigiza ikiwemo katika maeneo mbalimbali ya Serikali ili kuleta uhalisia mfano polisi, mahakamani na kwenye vivutio vya utalii na sehemu nyinginezo, tofauti na sasa hivi hata wakiomba vibali inakuchukua hata mwaka kuvipata.

Pia kwa wasanii anasema ni lazima wakubali kubadilika na kuachana na tabia ya kuchezea kazi zao jijini Dar es Salaam wakati Tanzania ni kubwa ambapo pia itawasaidia kutowachosha watazamaji wao kuona maeneo yaleyale kila siku.