Njombe yaibuka kidedea usafi wa mazingira

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu 

Dar es Salaam. Halmashauri ya mji wa Njombe kwa mara nyingine tena imeibuka kidedea katika mashindano ya Taifa ya afya na usafi wa mazingira yaliyohusisha halmashari za miji, majiji, manispaa na wilaya 73.

Katika shindano hilo halmashauri ya mji wa Njombe ilishika nafasi ya kwanza kwa kufanya vizuri katika uthibiti wa taka ngumu, usimamizi wa sheria , udhibiti wa maji taka, uwepo wa maji safi na salama pamoja na ushirikishwaji wa sekta binafi katika usafi wa mazingira.

Halmashauri ya Wilaya ya Njombe nayo ilishika nafasi ya pili katika kipengele cha utekelezaji wa kampeni ya Taifa ya usadi wa mazingira katika ujenzi na matumizi ya vyoo bora.

Njombe pia iliibuka kidedea katika kipengele cha kijiji bora chenye kaya ambazo zimefanikiwa kujenga na kutumia vyoo bora pamoja na sehemu za kunawia mikono kwa maji na sabuni nafasi iliyoshikwa na Kijiji cha Kanikele.

Akitangaza matokeo hayo Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ametoa wito kwa halmashauri nyingine kuiga mfano huo ili kuhakikisha mazingira yanakuwa safi na kuondoa uwezekano wa kutokea maradhi.

Amesema maeneo ambayo mazingira yake yako safi na watu wanatumia vyoo ni nadra kutokea magonjwa ya mlipuko.

“Asilimia 80 ya wagonjwa wanaokwenda hospitali kila siku wanatokana na magonjwa yanayosababishwa na mazingira kutokuwa safi, lazima tubadili fikra zetu na kulipa kipaumbele suala la mazingira,”

“Kufuatia ushindi huu wenzetu wa Njombe watapata gari la kubebea taka ili wakaendelee kuweka vizuri mazingira yao,”amesema