Sunday, October 22, 2017

Nkamia amfagilia JPM majadiliano na Barrick Gold

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi mwananchi@mwananchi.co.tz

Mbunge wa Chemba (CCM), Juma Nkamia amesema Serikali inastahili pongezi kwa majadiliano yake na kampuni ya Barrick Gold yanayohusu uwekezaji kwenye madini.

Alhamisi iliyopita, Rais John Magufuli alipokea ripoti ya mazungumzo kati ya Serikali na kampuni mama ya Acacia, Barrick Gold iliyoeleza makubaliano yaliyoafikiwa ili kuendelea na uchimbaji wa dhahabu nchini, ikiwamo kulipa Dola 300 milioni za Marekani (zaidi ya Sh660 bilioni).

Lakini siku moja baada ya taarifa hiyo, ofisa mwandamizi wa fedha wa Acacia, Andrew Wray alisema kampuni hiyo haina uwezo wa kulipa kiasi hicho.

Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa na vyombo tofauti vya habari vya kimataifa, uongozi wa Acacia umesema hauna uwezo wa kulipa kiasi hicho cha fedha.

“Hatuna huo uwezo kuilipa Tanzania ili tumalizane kwenye mgogoro wa kodi uliopo,” alikaririwa ofisa mkuu wa fedha wa kampuni hiyo, Wray.

Pamoja na changamoto zilizopo, Nkamia alisema hatua hiyo bila kujali tofauti ya itikadi kutokana na vyama vilivyopo, Watanzania wanapaswa kumpongeza Rais Magufuli.

“Serikali imefanya kazi nzuri. Hata kama humpendi mtu, mpongeze akifanya vizuri,” alisema Nkamia.

Miongoni mwa makubaliano ya Serikali na Barrick Gold ni kwamba sasa pande hizo mbili zitakuwa zikigawana faida asilimia 50 kwa 50.

-->