Nondo awasilisha barua ya kumkataa Hakimu Mpitanjia

Muktasari:

Kambole alidai ni haki ya mshtakiwa kumkataa hakimu kama anaona haki haitendeki.

Iringa. Mwanafunzi wa mwaka wa tatu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Abdul Nondo ameiandikia barua Mahakama ya Wilaya ya Iringa kumkataa hakimu John Mpitanjia anayesikiliza shauri lake.

Nondo ambaye pia ni mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi nchini (TSN), alisema anamtilia mashaka hakimu huyo hivyo ameona aiandikie barua mahakama ili itende haki.

Wakili wa Nondo, Jebra Kambole ndiye aliyewasilisha barua hiyo ambayo imeeleza kuwa kuna mazingira yasiyo rafiki katika kesi hiyo. Baada ya kuwasilisha malalamiko hayo, wakili wa Serikali, Abeid Mwanadalamo alidai kujiondoa kwa hakimu kutakubaliwa iwapo tu malalamiko yaliyoletwa ni ya msingi na ushahidi upo wazi.

“Kama aliona kuna kasoro alitakiwa alete malalamiko yake mwanzoni si leo,” alieleza.

Mwandalamo alieleza kuwa hizo ni njama za kutaka kuchelewesha shauri hilo na akaiomba mahakama kulitupilia mbali ombi hilo.

Kambole alidai ni haki ya mshtakiwa kumkataa hakimu kama anaona haki haitendeki.

Baada ya maelezo hayo, hakimu Mpitanjia aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 16 kwa ajili ya uamuzi.