Nsekela amrithi Dk Kimei CRDB

Abdulmajid Musa Nsekela.

Muktasari:

  • Bodi ya wakurugenzi wa CRDB imemtangaza kuiongoza benki hiyo

Dar es Salaam. Bodi ya CRDB imemtangaza Abdulmajid Musa Nsekela kurithi kiti cha mkurugenzi mtendaji wa benki hiyo, Dk Charles Kimei, kuanzaia Juni, 2018.

Nsekela anarudi kujiunga na Benki ya CRDB baada ya kuondoka kwa takriban muongo mmoja uliopita alipoihama benki hiyo na kujiunga na Benki ya NMB.

Taarifa iliyotolewa na mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa CRDB, Ally Laay leo Alhamisi Septemba 20, 2018  inasema mteule huyo ana ufahamu wa kutosha kusimamia na kuongoza taasisi za fedha na amekuwa mbunifu wa bidhaa na huduma tofauti kwa kipindi alichohudumu kwenye sekta hiyo.

“Nsekela ana uzoefu wa zaidi ya miaka 20 kwenye sekta ya benki; biashara na udhibiti,” inasomeka sehemu ya taarifa ya mwenyekiti huyo.

Mabadiliko hayo ya uongozi wa juu wa benki hiyo kubwa zaidi nchini yanafanyika kumruhusu Dk Kimei kupumzika baada ya kuingoza kwa takriban miaka 21.

Ndani ya uongozi wa mkurugenzi huyo, Nsekela alikuwa miongoni mwa waliochangia mafanikio ya taasisi hiyo kabla hajaondoka na kujiunga na NMB, wapinzani wa kibiashara kwenye sekta ya benki na fedha.

Taarifa ya Laay inabainisha kuwa Nsekela alijiunga na CRDB mwaka 1997 kama ofisa wa benki na miaka mitatu (2000) baadaye akapandishwa cheo na kuwa meneja uhusiano.

Kutokana na utendaji mzuri, miaka mitatu mbele (2003) aliongezewa majukumu na kuwa meneja uhusiano mwandamizi, nafasi aliyodumu nayo mpaka anaondoka na kujiunga na NMB mwaka 2008.