Nyalandu, Ole Nangole kupata warithi leo

Muktasari:

Wakati Nyalandu akijiuzulu, Ole Nangole wa Chadema alivuliwa wadhifa wa ubunge wa Longido na Mahakama kutokana na kasoro kadhaa zilizojitokeza kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Dar es Salaam. Warithi wa Lazaro Nyalandu, Leonidas Gama na Onesmo Ole Nangole wanatarajiwa kupatikana leo katika uchaguzi mdogo wa marudio wa majimbo matatu.

Majimbo hayo ni Singida Kaskazini (Singida), Songea Mjini (Ruvuma) na Longido (Arusha). Uchaguzi wa majimbo hayo unafanyika kutokana na sababu tofauti ambazo ni kujiuzulu ubunge, kifo na kutenguliwa na Mahakama.

Jimbo la Singida Kaskazini lilikuwa chini ya Nyalandu kwa muda mrefu lakini Oktoba mwaka jana alitangaza kujivua uanachama wa CCM na nyadhifa zake zote akisema haridhishwi na mwenendo wa siasa nchini.

Mbali na hilo, Nyalandu alimwandikia barua Spika wa Bunge, Job Ndugai akimweleza kwamba anajiuzulu wadhifa huo alioutumikia kwa vipindi vinne mfulululizo tangu alipochaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2000.

Baada ya kuchukua hatua hiyo, Nyalandu ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii katika Serikali ya Awamu Nne, alitangaza kuhamia chama kikuu cha upinzani cha Chadema.

Wakati Nyalandu akijiuzulu, Ole Nangole wa Chadema alivuliwa wadhifa wa ubunge wa Longido na Mahakama kutokana na kasoro kadhaa zilizojitokeza kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Jimbo la Songea Mjini nalo lilibaki wazi kutokana na kifo cha Gama aliyefariki dunia Novemba mwaka jana baada ya kuugua ghafla.

Tofauti na chaguzi nyingine ndogo zilizotangulia, uchaguzi wa leo hautarajiwi kuwa na ushindani kutokana na baadhi ya vyama vya upinzani vikiongozwa na Chadema kususia kwa sababu ya kasoro zilizojitokeza katika uchaguzi mdogo wa udiwani wa kata 43 uliofanyika Novemba 26 mwaka jana.

Akizungumza na wanahabari Desemba 11 mwaka jana, akiwa ameambatana na viongozi wenzake wa Ukawa, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema uchaguzi wa kata hizo uligeuka uwanja wa vita badala ya jukwaa la kuchagua viongozi na aliitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kuahirisha uchaguzi wa majimbo hayo matatu.

Mbowe alitaka majadiliano ya wadau ili kuondoa kasoro hizo hivyo kuwa na uchaguzi ulio huru na haki katika majimbo hayo matatu.

“Hatuwezi kushiriki uchaguzi wakati tumefungwa mikono, hii ni sawa na timu ya mpira kwenda kwenye mashindano bila kufanya mazoezi,” alisema Mbowe katika mkutano huo na wanahabari.

Hata hivyo, matakwa hayo yalitupiliwa mbali na NEC ambayo ilisema taratibu za uchaguzi huo upo kwa mujibu wa sheria na kama upinzani unadhani kuna kasoro ungeweza kwenda mahakamani kupinga.

Wakati Mbowe akieleza hayo, mwezi uliofuata Chama cha ACT-Wazalendo kupitia kwa mwenyekiti wake, Yeremia Maganja kilitangaza pia kususia ili kufikisha ujumbe kwa wadau wa siasa kuwa kuna tatizo hivyo kuwepo jana ya majadaliano.

Vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF, NLD, Chaumma na ACT-Wazalendo vimetangaza kususia uchaguzi huo, wakati CUF upande wa unaomuunga mkono mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba anayetambuliwa na ofisi ya Msajili ya Vyama vya Siasa, ukitangaza kushiriki uchaguzi huo.

Tayari Katibu wa Uenezi CCM Arusha, Shaaban Mdoe ameshaweka wazi ya kuwa chama hicho kitaibuka kidedea kwa asilimia 96 katika uchaguzi huo baada ya Chadema kuweka mpira kwapani.

Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma, upande wa Profesa Lipumba, Abdul Kambaya aliwataka wananchi wa majimbo na kata zinazorudia uchaguzi kujitokeza kwa wingi leo.

“Ingawa uchaguzi wa kata 43 ulikuwa una dosari kadhaa, lakini tumeona kususia siyo jambo jema.Kesho (leo) wananchi wajitokeza kwa wingi na kupiga kura na CUF itazilinda kwa mujibu wa taratibu,” alisema Kambaya.