Nyalandu aibuka upya Chadema, ataka wawe jasiri kuikabili CCM

Lazaro Nyalandu

Muktasari:

Nyalandu aliyetangaza kujivua ubunge na kuihama CCM Oktoba 30 mwaka jana kwa madai hafurahishwi na mwenendo wa siasa ndani ya chama hicho, kwa mara ya kwanza aliibukia katika mkutano wa ndani wa Chadema wilayani Tarime mkoani Mara na kuelezea siri ya ukimya wake.

Dar es Salaam. Baada ya takriban mwaka mzima wa ukimya, mbunge wa zamani wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu ameibuka upya akiwataka makada wa Chadema kuwa jasiri kuikabili CCM.

Nyalandu ndiye alikuwa mbunge wa kwanza kujivua ubunge na kuihama CCM na kutinga Chadema tangu Uchaguzi Mkuu 2015.

Alitangaza uamuzi wake huo Oktoba 30, 2017 akiwa jijini Arusha alisema hafurahishwi na mwenendo wa siasa ndani ya chama tawala.

Hata hivyo, Nyalandu hakugombea tena nafasi hiyo katika uchaguzi wa marudio ulioitishwa na tangu wakati huo amekuwa kimya.

Tangu aondoke CCM, tayari kuna wabunge tisa wa upinzani waliohamia CCM na kurudia ubunge wao katika majimbo waliyokuwa wanayaongoza au wakisubiri uchaguzi.

Wabunge hao ni pamoja na Maulid Mtulia (Kinondoni), Dk Godwin Mollel (Siha), Mwita Waitara (Ukonga), Julius Kalanga (Monduli) na Zuberi Kuchauka (Liwale) ambao tayari chaguzi zimeshafanyika na wamerejea bungeni.

Wengine ni aliyekuwa Mbunge wa Serengeti Chacha Ryoba, Joseph Mkundi wa Ukerewe, James Millya wa Simanjiro na Pauline Gekul wa Babati Mjini. Wabunge hao wote ni wa Chadema isipokuwa Mtulia na Kuchauka waliotokea CUF.

Mbali na wabunge hao, madiwani na makada kadhaa wamevihama vyama vya upinzani na kwenda CCM wakisema wanaunga mkono juhudi za Rais John Magufuli.

Nyalandu na Biblia

Akizungumza hivi karibuni katika mkutano wa ndani wa Chadema uliofanyika wilayani Tarime, Mkoa wa Mara, Nyalandu aliyekuwa akitumia maandiko ya Biblia alitoa mfano wa mtu aliyeitwa Bathlomayo aliyekuwa kipofu aliyeponywa na Yesu Kristo.

“Waheshimiwa wapiganaji wenzangu, mimi ni yule tuliyesoma wote kidato kimoja, mimi ni yule ambaye nilisimama katika siku ambayo hawakutarajia na pengine nyie hamkutarajia, baada ya kutafakari sana nikaondoka,” alisema Nyalandu huku akishangiliwa na makada wa chama hicho.

Aliendelea, “Baada ya mwaka mmoja, maana watu waliuliza Nyalandu yuko wapi, maana alikuja halafu akapotea. Nikawaambia watu kulikuwa na saa ambayo ni lazima ifike na hiyo saa ilikuwa jana. Ilikuwa ni mara ya kwanza kuvaa gwanda, kukaa ngangari na kuwa tayari kwa ajili ya hili zoezi (kazi).”

Akisimulia kisa cha kipofu Bathlomayo, alisema mtu huyo aliposikia mtu mkubwa (Yesu) anapita eneo hilo alipiga kelele akitaka aponywe upofu wake.

“Alichokifanya, akasikia mkubwa anakuja kama hivi (Freeman) Mbowe (Mwenyekiti wa Chadema). Akakaa barabarani akimsubiri yeye alikuwa kipofu, ukiwa kipofu huoni lakini unaweza kusikia, alikuwa anasikia mambo yanakuja, mageuzi yanakuja. Akakaa barabarani.”

Nyalandu alisema Watanzania wengi wanatembea wakiwa vipofu kwa sababu hawaoni dhuluma wanazofanyiwa. “Kwa sababu kama mtu anaona kulikuwa na dhuluma anaiona waziwazi, kama kulikuwa na kunyanyasika anaguswa na kuona kinachotokea anafanya uamuzi tofauti,” alisema mwanasiasa huyo.

Enzi zake CCM

Akizungumzia enzi zake akiwa CCM, Nyalandu alisema walikuwa wakiwaogopa Chadema na walipanga mengi ya kupambana nao, hivyo akawataka makada hao kutokiogopa chama tawala.

“(Zamani) Tukisikia Chadema, Bavicha wanakuja hatulali tunajipanga. Tulikuwa tunawaogopa, tunasema hawa jamaa wanakuja na wanajielewa,” alisema.

“Ester Bulaya alikuja siku moja tulikaa mpaka saa tisa usiku tunapanga mipango ya kuwashughulikia Chadema.” Hata hivyo alishangazwa kuona Chadema wameanza kuwa waoga tofauti na zamani wakiogopa hata kuvaa sare zao.

Makada wa upinzani na wabunge

Aliwaponda wabunge na makada wa upinzani wanaohamia CCM akisema wanawadanganya wananchi wanaposema wanaunga mkono juhudi. “Labda wengi na wabunge wanaohama badala ya kurudi kishujaa unaondoka kuunga juhudi ambazo hazipo, unamdanganya nani? Unaidanganya jamii au unadanganya watu.”

Nyalandu aliwataka makada wa Chadema kusimama imara kama mashujaa huku wakiwaona Watanzania kama watu halisi kama alivyoona Bathlomayo baada ya kuponywa. “Utashangaa CCM tulikuwa tunawaogopa, nyie mnafikiri tulikuwa hatuwaogopi. Kumbe ‘una -deal’ na waoga watupu, ‘una-deal’ na watu ambao hawana kura kabisa. Kwa hiyo ndiyo maana wanawatia ndani, lazima wawatie chokochoko ili mashujaa wakipigwa watu wakimbie, watu wanaogopa, ushindi uko mikononi mwenu.”

Awali, akihutubia mkutano huo, mwenyekiti wa Chadema, Mbowe alisema kihistoria chama hicho kilianza kikiwa na ng’ombe wanne ambayo ni maeneo ya Kilimanjaro, Kigoma, Karatu na Tarime lakini sasa kimepata mafanikio makubwa.

“Nashukuru kwa sababu yale mapenzi ya chama yaligeuzwa kuwa maendeleo ya watu. Tulionekana kwamba sisi ni watu wa mikutano na maandamano, wenzetu wakatubeza na kutudhalilisha,” alisema Mbowe.

Wavamia Kanda ya Ziwa

Nyalandu ametoa tamko lake wakati Chadema imeanza mikutano yake ya ndani kwa viongozi wao kugawana maeneo ya Kanda ya Ziwa. Katika mgawanyo huo, timu ya Mbowe itakuwa Mwanza mjini, wakati ile ya katibu mkuu, Dk Vincent Mashinji ikiwa wilayani Rorya na naibu katibu mkuu (Bara), John Mnyika yuko Geita mjini huku ile ya naibu katibu mkuu (Zanzibar), Salum Mwalimu ikiwa wilayani Mbogwe mkoani humo.

Timu nyingine inaongozwa na waziri mkuu mstaafu, Frederick Sumaye iko wilayani Serengeti huku mbunge wa Kawe, Halima Mdee na wa Bunda, Ester Bulaya wakiikabili Wilaya ya Ukerewe.