Nyanduga: Haturidhishwi na ulinzi wa haki za wenye ualbino

Muktasari:

Pia, imesema kesi zinazohusu mauaji ya albino na vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu zinachukua muda mrefu kutolewa uamuzi.

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, imesema hairidhishwi na namna haki za watu wenye ulemavu wa ngozi zinavyolindwa nchini.

Pia, imesema kesi zinazohusu mauaji ya albino na vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu zinachukua muda mrefu kutolewa uamuzi.

Mwenyekiti wa tume hiyo, Bahame Nyanduga amesema hayo leo (Jumatatu) kwenye mdahalo wa kupinga vitendo vya uvunjifu wa haki za watu wenye ulemavu wa ngozi ambao umehudhuriwa na wadau kutoka Shirika la Under The Same Sun (UTSS), jamii ya watu wenye ulemavu wa ngozi (Tas) na wawakilishi kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

Amesema kumekuwapo vitendo vya baadhi ya watu kufukua makaburi ya watu wenye ulemavu wa ngozi kwa imani za kishirikina, ubaguzi na unyanyapaa kwenye jamii.

“Tungekuwa tumeridhika na namna haki za watu hawa zinavyolindwa tusingekuwa hapa na mdahalo huu, ukiona hivyo ujue bado. Tunatoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi kuhusu watu wanaojihusisha na vitendo vya kikatili dhidi ya albino,” amesema.

Wakili wa Serikali, Beatrice Mpangala amesema kuanzia mwaka 2006 mpaka sasa jumla ya kesi 66 zimeripotiwa kwenye ofisi ya DPP.

Amesema kati ya hizo, mashauri 55  yanaendelea kwenye mahakama mbalimbali nchini na 11 bado ushahidi haujakamilika kutokana na upande wa mashtaka kukosa ushahidi wa kutosha.

“Mara nyingi matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi hufanyika usiku, hivyo inachukua muda kwa polisi kupata ushahidi wa kutosha,” amesema.

Mpangala amesema ofisi ya DPP inafanya kazi kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi na UTSS kwa lengo la kupata ushahidi wa kesi hizo. “Tunaomba wananchi wasaidie Jeshi la Polisi kutoa taarifa za watu wanaohusika na vitendo hivyo ili ofisi yetu iweze kuchukua hatua za kisheria.”

Mkurugenzi Mtendaji wa UTSS, Peter Ash amesema bado watoto wenye ulemavu wa ngozi hawajapewa kipaumbele na hasa kupatiwa vifaa vya kuwakinga na jua ili wasipate saratani ya ngozi.

Pia, alishauri Serikali kama ina nia ya kumaliza tatizo hilo ni lazima iwekeze vya kutosha katika kutoa elimu kwa wananchi juu ya kulinda haki za watu wenye ulemavu wa ngozi ili waweze kuishi kwa amani.