Nyani azima umeme kwa saa 6 Zambia

Lusaka, Zambia. Mafundi umeme na ‘vishoka’ ndio wenye uwezo wa kukata umeme katika eneo fulani kwa ajili ya matengenezo lakini katika mji wa Livingstone nchini Zambia, nyani alikata umeme na kuathiri watumiaji wapatao 50,000

Nyani huyo alifanikiwa kuingia katika kituo cha umeme jana na kuvuruga mitambo inayosambaza umeme kwenda maeneo ya Kusini na magharibi mwa Zambia, kwa mujibu wa kampuni ya umeme nchini humo, Zesco.

Taarifa ya shirika la umeme la Zambia imesema wakazi 28,000 wa Livingstone na watu wengine 22,000 wa eneo hilo walibaki bila umeme kwa zaidi ya saa sita wakati ukarabati ukiendelea.

"Nyani huyo alipigwa na umeme lakini kutokana na maumbile yake ya kimazingira alipata tu majeraha mabaya ya moto. Kama angekuwa binadamu angekufa," imesema Zesco.

Zesco imewaomba msamaha wateja wake kwa hasara waliyoipata.

Mji wa Livingstone ni maarufu kwa wanyama pori kama nyani na ndovu wanaotoka mbuga iliyo karibu na mji huo.