Saturday, November 18, 2017

Nyara za Serikali zawafikisha kortini

 

By Anthony Mayunga, Mwananchi amayunga@mwananchi.co.tz

Serikali imewapandisha kizimbani wakazi wawili wa vijiji vya Biashara na Kisangura wilayani hapa mkoani Mara kwa tuhuma za kukutwa na nyara za Serikali zenye thamani ya Sh69 milioni.

Washtakiwa hao ni Masoba Chacha (27) mkazi wa Bisarara na Mwita Maka (25) mkazi wa Kisangura ambao walikamatwa Novemba 10, 2017 saa kumi jioni, eneo la Mto Rangi ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi, Amalia Mushi, mwendesha mashtaka wa Serikali, Shukran Msuya alidai kuwa washtakiwa hao wanakabiliwa na makosa matano.

Alidai kuwa kosa la kwanza ni kuingia ndani ya hifadhi ya Taifa bila kibali na la pili ni kukutwa na sime mbili, waya sita na visu viwili.

Kosa la tatu ni kukutwa na vipande viwili vya nyama kavu na ngozi vya swala zenye thamani ya zaidi ya Sh8 milioni.

Pia, alidai kuwa kosa la nne walikamatwa na vipande vinne vya nyama ya pundamilia vyenye thamani ya zaidi ya Sh27 milioni kinyume cha sheria.

Mwendesha mashtaka aliiambia Mahakama kuwa kosa la tano ni kukutwa na vipande viwili vya ngozi ya twiga vyenye thamani ya zaidi ya Sh34 milioni.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 27 washtakiwa watakaposomewa masharti ya dhamana.

-->