Nyaraka za Manji zasalimika uvamizi ofisi za mawakili Dar

Muktasari:

Hata hivyo, nyaraka za kesi ya mfanyabiashara huyo zimesalimika, huku msemaji wa ofisi hiyo wakili Asia Charli akisema licha ya jengo hilo kuwa na ofisi mbalimbali kama maduka, saluni na gym ni ofisi yao tu iliyopo ghorofa ya tatu ndiko kumeibwa nyaraka na fedha.

 Watu wasiojulikana waliovunja ofisi za mawakili wa Prime Attorneys ambayo pia inashughulikia kesi ya Yusuf Manji wameiba Sh3.7 milioni na nyaraka kadhaa zikiwamo hati za viwanja.

Hata hivyo, nyaraka za kesi ya mfanyabiashara huyo zimesalimika, huku msemaji wa ofisi hiyo wakili Asia Charli akisema licha ya jengo hilo kuwa na ofisi mbalimbali kama maduka, saluni na gym ni ofisi yao tu iliyopo ghorofa ya tatu ndiko kumeibwa nyaraka na fedha.

Ofisi za kampuni hiyo zipo jengo la Prime House lililopo Mtaa wa Tambaza, Upanga jijini Dar es Salaam jirani na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wilayani Ilala.

Katika wizi huo, watu hao wasiojulikana waliiba kasiki lenye fedha na nyaraka.

Hilo ni tukio la pili kwa ofisi za mawakili katika siku za karibuni kufanyiwa uhalifu, baada ya kampuni ya Immma Advocates kushambuliwa na kitu kilichodaiwa kuwa bomu na kuteketea kwa baadhi ya nyaraka.

Akizungumzia tukio la kuibwa kwa fedha na nyaraka katika ofisi yao, Charli alisema jana kuwa: “Nyaraka mbalimbali za wateja na zetu zimechukuliwa na ni za muhimu sana.” Alisema nyaraka kuhusu kesi za mfanyabiashara Manji anayewakilishwa na kampuni hiyo zilisalimika.

Wakili katika ofisi hiyo, Hudson Ndusyepo ambaye ni miongoni mwa mawakili wanaomtetea Manji katika kesi ya uhujumu uchumi, alisema kabla ya wizi huo waliohusika walimfunga kamba mlinzi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Salum Hamduni alisema tukio hilo lilitokea kati ya saa nane na tisa usiku wa kuamkia jana na uchunguzi unaendelea.

Katika tovuti yake, Prime Attorneys inaeleza kuwa ilianzishwa mwaka 2010.

Awali jana asubuhi mwandishi wa Mwananchi alishuhudia barabara ya kuingia zilipo ofisi za kampuni hiyo ikiwa imefungwa kwa muda na polisi ambao walitumia magari yao kuziba njia na kuweka uzio wa utepe wa rangi ya njano.

Mmiliki wa saluni ya Posh Unisex, Fatma Ebrahim alisema katika uvamizi huo, pia mlango wa saluni yake wenye thamani ya Sh2.5 milioni ulivunjwa lakini hakuna mali iliyoibwa.

Kwa sasa siwezi kusema wahalifu hawa walilenga ofisi gani maana zipo nyingi katika jengo lile. Naomba mtupe nafasi tufanye uchunguzi kisha tutawapa taarifa