Nyuma ya pazia Kakonko kuwa wilaya maskini zaidi

Muktasari:

Wakati akitoa Mpango wa Maendeleo kwa Mwaka 2016/17 Juni mwaka jana, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango aliitaja Kakonko iliyopo mkoani Kigoma kuwa ni wilaya maskini ambayo asilimia 60 ya watu wake wanaishi chini ya mstari wa umaskini wa mahitaji ya msingi

Kakonko. Miezi saba baada ya Kakonko kutajwa kuwa ni wilaya maskini zaidi nchini, gazeti hili limebaini sababu zilizofanya halmashauri hiyo kutopea katika hali hiyo na namna viongozi wanavyokabiliana nayo.

Wakati akitoa Mpango wa Maendeleo kwa Mwaka 2016/17 Juni mwaka jana, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango aliitaja Kakonko iliyopo mkoani Kigoma kuwa ni wilaya maskini ambayo asilimia 60 ya watu wake wanaishi chini ya mstari wa umaskini wa mahitaji ya msingi. Wilaya hiyo ina sifa sanjari na Biharamulo iliyopo mkoani Kagera. Mahitaji yao ya msingi ni chakula, mavazi na malazi.

Hata hivyo, uchambuzi wa takwimu za umma na uchunguzi uliofanywa na mwandishi wetu unaonyesha kuwa pamoja na hali mbaya kiuchumi, bado wilaya hiyo ina fursa lukuki zinazoweza kuifanya kuwa miongoni mwa maeneo tajiri nchini.

Tofauti na baadhi ya wilaya au manispaa zilizoendelea nchini, takwimu za Sensa ya Watu ya Mwaka 2012 zinaonyesha kuwa sehemu kubwa ya wakazi 167,555 wa Kakonko, wanaishi vijijini wakijushughulisha zaidi na kilimo. Ni watu watatu pekee kati ya 100 wanaoishi mjini.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, watu 83 kwa kila 100 waliopo wilayani humo hujishughulisha na kilimo na waliosalia wakijipatia riziki kwa kufanya kazi nyingine kama biashara, useremala, ufundi uashi, uvuvi katika mito na kuajiriwa katika sekta rasmi na binafsi.

 

Kwa nini ni maskini?

Umaskini huo wa Kokonko unatokana na mwenendo halisi wa kipato chao.

Kipato cha mwananchi wa kawaida wa Kakonko kwa mujibu wa tovuti ya wilaya hiyo, kinakadiriwa kuwa ni wastani wa Sh500,821 kwa mwaka kwa hesabu ya mwaka 2011. Hii inamaanisha kuwa mwananchi wa kawaida hupata Sh41,735 kwa mwezi sawa na Sh1,391 kwa siku.

Kiwango hicho kipo chini mara tatu ya kipato cha dola 1.9 za Marekani kwa siku (sawa na Sh4,100) kinachopendekezwa na Benki ya Dunia (WB) ili kuvuka mstari wa umaskini wa kutopea.

 

Umaskini Kakonko si bahati mbaya

Kakonko ni moja ya wilaya changa nchini iliyoanzishwa miaka minne iliyopita baada ya kumegwa kutoka Wilaya ya Kibondo.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Kakonko, Simon Mando anasema kabla ya kupata hadhi hiyo, “Hapakuwa na gesti wala benki, watu wengi walikuwa wanaweka fedha Kibondo”.

Anasema baada ya kupewa hadhi hiyo, ofisi anayotumia sasa ilikuwa ni ya ofisa mtendaji wa kata, ofisi ya mkuu wa wilaya ilikuwa ni ofisi ya ofisa tarafa na ofisi ya wakuu wa idara ilikuwa ni ofisi ya halmashauri ya kijiji.

 

Fedha za Tasaf zatumika kunywea

Umaskini wa wilaya hiyo umeulazimu Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) kuingiza robo ya kaya 33,511 za Kakonko, katika mpango wa kunusuru kaya maskini. Hata hivyo, si fedha zote zinatumika kwenye matumizi yaliyokusudiwa.

Tasaf inaeleza kuwa mwaka 2015 wilaya hiyo ilikuwa na kaya 8,006 maskini zilizokuwa zikipata fedha hizo, lakini hadi kufikia Novemba mwaka jana zilipungua hadi kufikia kaya 7,839 kutokana na baadhi wazee kuchukuliwa na watoto wao walioko mijini na wengine kuihama wilaya hiyo.

Kaimu ofisa wa Tasaf wilayani Kakonko, Jabir Timbako anasema vijiji 32 kati ya 44 vimo ndani ya mpango huo unaolenga kuwawezesha wananchi kiuchumi ili waondokane na umaskini uliotopea.

“Zipo baadhi ya kaya zikipata mlo mmoja ndiyo basi tena, hivyo tumeziangalia na tumekuwa tukizipa fedha na kuzitaka zianzishe walau kitu ili ziweze kujiendeleza,” anasema Timbako, ambaye pia ni ofisa maendeleo ya jamii.

Anasema mpango huo wa Tasaf umezisaidia kaya hizo kwa kuwa hata mahudhurio ya watoto yameongezeka shuleni na pia kina mama wajawazito wamekuwa wakihudhuria kliniki.

Licha ya Serikali kuziwesha kaya hizo maskini, bado kuna wananchi ambao wamekuwa wakizitumia kwa malengo ambayo hayajakusudiwa na mipango huo.

Timbako anasema kuna baadhi ya wazee wa familia ambao wakipata fedha hizo, huzitumia kunywa pombe badala ya kuzifikisha nyumbani.

Timbako anasema maisha ya Kakonko si ghali, lakini kinachoathiri ni kuwa mpakani na Burundi ambako hakujatulia kisiasa.

Kama zilivyo wilaya nyingine katika nchini zinazoendelea, Kakonko ina tatizo la miundombinu na huduma muhimu za kijamii kama umeme, maji na afya.

Barabara zote zinazopita wilaya hiyo ni za vumbi. Lami kwao ni “anasa”.

Ili kufika Kakonko kwa mtu anayetokea Dar es Salaam, inachukua siku mbili kutokana na ubovu wa barabara, hususan kuanzia Nyakanazi mkoani Kagera.

Baadhi ya malori yanayopeleka mizigo Kakonko kutoka Kahama, Mwanza, Bukombe na kwingineko yalionekana kukwama katika maeneo tofauti ya barabara hiyo na wakati mwingine kufanya mabasi ya abiria kusimamisha safari kwa muda ili kusubiri yaondolewe katika tope.

Miundombinu isiyo rafiki imeathiri pia mwenendo wa biashara wilayani Kakonko ambayo inapakana na Burundi kwa upande wa Kaskazini na Magharibi.

 

Wafanyabiashara wanena

Hamis Selemani ambaye pia ni mmiliki wa mabasi yanayofanya safari zake kati ya Kakonko na maeneo mengine, anasema ubovu wa barabara hiyo umekuwa changamoto kipindi cha mvua.

“Pamoja na kwamba kwa sasa barabara imeanza kujengwa, lakini imetucheleweshea kukua kibiashara kwa kuwa abiria anapotokea Nyakanazi kwenda Kakonko, Kibondo hadi Kasulu huchukua muda mrefu njiani kutokana na ubovu.

“Hii inapunguza pia idadi ya safari na kusababisha kupunguza ukuaji wa biashara,” anasema Selemani.

Hata hivyo, pamoja na takwimu kuonyesha Kakonko ni wilaya maskini zaidi nchini, bado sehemu ya wananchi wake wana nyumba bora zilizoezekwa bati na kujengwa kwa matofali ya kuchoma.

Ukiingia tu wilaya hiyo kutokea Nyakanazi, utaona jinsi wakazi walivyojenga nyumba kwa matofali ya kuchoma zikiwa zimezungukwa na miti mingi mirefu.

Mkazi wa Kakonko, Johnson Kahigi anasema habari kwamba wilaya yao ni maskini ziliwashangaza kwa kuwa hawajui walitumia takwimu gani.

Anasema habari hizo zinawashusha morali wa kufanya kazi zao kwa kuwa licha ya wilaya hiyo kuwa changa, kuna maendeleo katika baadhi ya maeneo.

 

Fursa lukuki

Tofauti na wilaya nyingine zenye eneo dogo la kilimo, Kakonko ina kilomita za mraba 1,084.2 za ardhi inayofaa kwa kilimo na takriban theluthi mbili ya eneo hilo linalimwa.

Kuna kilomita za mraba 806.4 zilizotengwa kwa malisho ya mifugo, eneo ambalo ni zaidi ya robo tatu ya lile lilopo kwa ajili ya kilimo.

“Hizo takwimu kwamba Kakonko ni maskini sijui ni za wapi. Watu wa Kakonko wana nyumba na zimeeezekwa kwa bati na kujengwa kwa matofali ya udongo, hata njaa hakuna ila wachache walio maskini pombe ndiyo tatizo,” anasema Mando.

Anasema kuwa suala la Kakonko kuwa ni maskini huenda limetokana na takwimu kuchukuliwa mapema wakati ikiwa changa, lakini kiuhalisia ina fursa lukuki ambazo wawekezaji wanakaribishwa kuzitumia ili kuchangia maendeleo ya halmashauri hiyo.

“Kilimo cha mihogo kinafanyika na hununuliwa hata nje, kilimo cha mpunga kinafanyika. Ni zao la biashara, ufugaji wa nyuki pembezoni mwa Pori la Moyowosi. Asali ipo na ni bora nje ya nchi kwa kuwa imefanyiwa utafiti,” anasema Mando.

 

Inajikokota kibiashara

Kwa miaka zaidi ya mitatu iliyopita, Kakonko imekuwa ikipambana kuongeza wigo wa mapato kwa kuchochea biashara baada ya awali kuwa na wafanyabiashara wachache.

Ofisa Biashara wa Wilaya, Erasmo Kishongoli anasema wakati inaanzishwa Novemba 2013 ilikuwa na wafanyabiashara 324 wa kati ambao hawakutosha kunenepesha mfuko wa mapato.

Hata hivyo, Kishongoli anasema urasimishaji wa biashara uliofanywa mwanzoni ulisaidia kuongeza wafanyabiashara wa kati hadi kufikia 618 katika mwaka 2015/16.

Uwepo wa idadi ndogo ya wafanyabiashara umesababisha halmashauri hiyo pia kukusanya mapato kidogo yatokanayo na ushuru wa biashara wakianzia na Sh9.8 milioni kwa mwaka 2013/14.

Kishongoli anasema mapato hayo yalipanda na kufikia Sh18.8 milioni mwaka 2015/16 ikiwa ni ongezeko la asilimia mia.

Anasema biashara inakua na sasa wafanyabiashara wanafungua vituo vya mafuta na ghala la kuhifadhia vinywaji.

Pia anasema shule za kisasa zimeanza kujengwa Kakonko hivyo kwa sasa mtu mwenye mtaji au anayetaka kufanya biashara, wilaya hiyo ni sehemu sahihi ya kuwekeza.

“Uwepo wa halmashauri umesaidia kuiinua Kakonko,” anasema Kishongoli.

Pamoja na kuwa katika mapambano ya kujikwamua na umaskini, wilaya hiyo ina rekodi ya kuwa na matatizo ya kiufanisi katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo.

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2014/15, inaitaja Kakonko kuwa ni miongoni mwa halmashauri saba zenye miradi yenye upungufu ambao uliigharimu wilaya hiyo zaidi Sh152 milioni.

Halmashauri nyingine ni jiji la Mbeya, Tanga, Musoma, Muleba, Sikonge na Ukerewe.