Nyumba Dodoma rangi moja

Muktasari:

  • Utaratibu huo utailazimu kila kata, miongoni mwa kata 41 za manispaa hiyo kuwa na rangi yake maalumu tofauti na nyingine.

Manispaa ya Dodoma imeanzisha utaratibu mpya utakaowalazimu wakazi wa eneo hilo kutumia rangi za aina moja kupaka kwenye mapaa ya majengo yao.

Utaratibu huo utailazimu kila kata, miongoni mwa kata 41 za manispaa hiyo kuwa na rangi yake maalumu tofauti na nyingine.

Kwa msingi huo, kila kata itakuwa na rangi moja itakayotumika kwa wakazi wote wa eneo hilo katika mapaa yao ya nyumba.

Diwani wa Kata ya Kizota, Jamal Yaledi amesema Baraza la Madiwani la Manispaa ya Dodoma ndio lilipitisha mpango huo.

Alisema walipitisha mpango huo uanze Machi lakini waliokwamisha ni wafanyabiashara ambao hawajaleta rangi za mabati.

“Tulipitisha mpango huo kwenye kikao cha robo ya pili ya mwaka cha Januari, lakini wafanyabiashara ambao ndiyo wadau wakubwa, wameshindwa kuleta rangi za mabati zinazotakiwa kwa wakati na hivyo kukwamisha kazi nzima,” alisema Yaledi.

Alisema ambao wameshajenga kwa kutumia mabati meupe wanashauriwa kuyapaka rangi kutokana na rangi ya kata husika.

Tangazo lililobandikwa ofisi za Manispaa mjini Dodoma linaonyesha mpangilio wa kila kata na rangi itakayotumika. Pia, tangazo hilo linaonyesha ramani inayoonyesha jinsi mji wa Dodoma utakavyoonekana kwa juu, baada ya utaratibu huo kukamilika.

Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa, Godwin Kunambi hakupatikana jana ila taarifa zilisema yupo kwenye mkutano.

Alipopigiwa simu yake ya mkononi ilipokelewa na msaidizi wake aliyejitambulisha kwa jina moja la Masanja ambaye alisema mkurugenzi huyo yuko kwenye kikao.

Ofisa Habari wa Manispaa ya Dodoma, Ramadhani Juma alisema utekelezaji wake bado haujaanza. “Mpango huo umepitishwa kwenye vikao halali vya baraza la madiwani Januari, lakini utekelezaji wake bado haujaanza,”alisema.

Hata hivyo, diwani wa Kata ya Viwandani (CCM), Jafar Mwanyembe alisema ingawa hana uhakika kama lilipitishwa na baraza la madiwani, wazo hilo ni la kibaguzi.

“Kama litatekelezwa ina maana ukienda Nkhungu unakutana na rangi fulani, ukienda Kiwanja cha Ndege unakutana na rangi fulani, hii ni ubaguzi sana,”alisema Mwanyemba, meya wa zamani wa manispaa hiyo.

Alisema kama utaratibu huo utatekelezwa ni wazi kwamba itabidi wawasiliane na mamlaka ya Kiwanja cha Ndege ambacho kitashauri ni rangi gani itumike katika maeneo ya karibu ili kuwezesha shughuli zake kutoathiriwa na mpango huo.

“Leo Manispaa ya Dodoma ina kata 41 kwani rangi zilizopo ni ngapi za kutosha kata zote? Kama suala hili lilipitishwa na madiwani wenzangu nasema kuwa ni bahati mbaya sana,”alisema.

Alisema hata gharama za kubadilisha rangi katika mapaa ya nyumba hazijadiliwi na zitawatia katika matatizo familia masikini.