NYANZA: Nyumba za nyasi zageuka fursa kwa viwanda vya mabati

Muktasari:

  • Wananchi wa mikoa husika watakiwa kuchangamkia ujio huo

Mwanza.  Zaidi ya asilimia 100  ya nyumba za kaya 2,081,045 za mikoa ya Kanda ya Ziwa bado zimeezekwa kwa nyasi, hali inayoonekana kuvutia wawekezaji wa viwanda vya kutengeneza mabati kutumia fursa hiyo. Kanda ya Ziwa inaundwa na mikoa ya Mwanza, Kagera, Mara, Shinyanga, Geita na Simiyu.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012, Mwanza ilikuwa na nyumba za kaya 481,107 huku asilimia 25.3 zikiwa zimeezekwa kwa nyasi.

 Kagera ni mkoa ambao ulionekana kuwa na nyumba nyingi zilizoezekwa kwa bati, kati ya 521,028 ni asilimia 23.8 zikiwa za nyasi.

Idadi ya mikoa mingine huku nyumba za nyasi kwa asilimia kwenye mabano ni Shinyanga 258,981 (27.8); Simiyu 227,862 (10.1); Mara 308,483       (34.3); na Geita 283,584 (29.1).

Ujenzi wa viwanda

Kutokana na uwapo wa soko, tayari Kampuni ya Alaf inayotengeza mabati imejenga kiwanda jijini Mwanza lengo likiwa ni utekelezaji wa sera ya Tanzania ya viwanda. 

Akifungua kiwanda hicho kilichojengwa Kata ya Igogo juzi,  Kiongozi wa mbio za mwenge, Amour Hamad Amour alipongeza uongozi wa kampuni hiyo kwa  kutumia fursa ya soko.

“Nitumie fursa hii kuwataka wawekezaji wengine kuja Mwanza kuwekeza, wala msiogope kwa sababu Serikali inatambua na kuheshimu uwapo wenu,” alisema.

Aliutaka uongozi wa Wilaya ya Nyamagana na Halmashauri ya Jiji la Mwanza kuendelea kuimarisha uhusiano mzuri na wawekezaji.

Pia, Amour aliwataka wakazi   wa Mwanza kuchangamkia fursa hizo hasa kupitia sekta ya viwanda, ili kuongeza soko la ajira kwa vijana.

Awali, akisoma taarifa ya kiwanda, Daud Kilyama ambaye ni mfanyakazi alisema hadi kukamilika kimegharimu Sh4.5 bilioni.

Kilyama alisema kiwanda hicho chenye wafanyakazi wanane wenye mikataba ya ajira za kudumu, vibarua wasiopungua 30 na watoa huduma mbalimbali 100, kimeanza uzalishaji mwaka huu  lengo likiwa ni kusogeza huduma karibu zaidi na wateja.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mary Tesha alisema ofisi yake ina uhusiano mzuri na uongozi wa kiwanda hicho na kwamba, tayari kimekubali kutoa mchango wa mabati kwa ajili ya ujenzi wa kituo kidogo cha polisi  Kata ya Luchelele.

Mwenge huo ulipokewa wilayani hapa Agosti 20 katika Kata ya Igoma, ukitokea wilayani Magu. Miradi 10 yenye thamani ya Sh7.2 bilioni wilayani Nyamagana itazinduliwa au kuwekwa mawe ya msingi.