VIDEO: Obama aahidi kusaidia sekta ya utalii nchini

Muktasari:

  • Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi Augustine Mahiga alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari baada ya kuzungumza faragha na Obama kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia).

Arusha. Rais mstaafu wa Marekani, Barack Obama ameeleza kuridhishwa na vivutio vya utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi Augustine Mahiga alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari baada ya kuzungumza faragha na Obama kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia).

Dk Mahiga alisema Obama ameahidi kuisaidia Tanzania kuvutia wawekezaji katika hifadhi hiyo ambayo pamoja na familia yake, Rais huyo mstaafu wameitembelea kwa wiki nzima.

Waziri Mahiga akizungumzia usiri wa ziara ya Obama aliyeondoka nchini jana mchana kwenda Kenya, alisema ni kutokana na kuwa ilikuwa ya binafsi.

“Alikuja kutembelea hifadhi ya Serengeti kwa safari binafsi, hivyo ni lazima tuheshimu hilo,” alisema.

Balozi Mahiga alisema Rais John Magufuli amempa Obama zawadi ya picha maalumu ya tukio la nyumbu wahamao katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambalo ni la kipekee duniani.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira aliyekuwapo Kia alisema ziara ya Obama na familia yake itaitangaza vyema Tanzania katika utalii.

Meneja uhusiano wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Pascal Shelutete alisema ziara ya Rais huyo wa zamani wa Marekani inatokana na jitihada za uhifadhi na kutangazwa vyema kwa bvivutio vilivyopo nchini.

“Ujio wa watalii wengi maarufu ni kazi nzuri inayofanywa na Tanapa na Serikali kutangaza vivutio vya utalii,” alisema Shelutete.

Kaimu mkurugenzi wa uwanja wa Kia, Christopher Mukoma alisema kwa Obama kutumia uwanja huo kunadhihirisha ubora wake.

Rais mwingine yupo

Baada ya Obama kuondoka, imeelezwa kuwa Rais wa Uswisi, Alain Berset na familia yake wapo nchini kutembelea vivutio vya utalii.

Waziri Mahiga alisema kiongozi huyo atakuwa nchini kwa siku 10 na kwamba, atakuwa Tanzania Bara kwa siku tano na nyingine Zanzibar.

Alisema kiongozi huyo atatembelea hifadhi za Taifa za Serengeti na Ngorongoro kabla ya kwenda Zanzibar.