Obama amfungulia njia Hillary Clinton

Rais Obama akiwa na mgombea wa Democratic, Hillary Clinton.Picha na AFP.

Muktasari:

Democratic yahitimisha mkutano wa kihistoria huku ikifanikiwa kuwatuliza wafuasi wa Bernie Sanders

Philadelphia, Marekani. Mgombea wa urais wa Chama cha Democratic nchini Marekani, Hillary Clinton jana aliweka rekodi kwa kutoa hotuba iliyowasisimua wengi, akiahidi kuendeleza mafanikio yaliyofikiwa na Rais Barack Obama.

Clinton akimkosa mpinzani wake wa Republican, Donald Trump, akisema yuko mbioni kuandika historia ya kuwa rais wa kwanza mwanamke Marekani.

Clinton aliyasema hayo wakati akifunga mkutano wa chama chake uliofanyika kwa siku nne Philadelphia.

Alisema Marekani ni Taifa kubwa na sasa linajiandaa kuandika historia kwa kumweka madarakani rais mwanamke na kwamba ataimudu nafasi hiyo.

Watu wengi wanasema hotuba ya Clinton imemaliza mgawanyiko uliokuwa umejitoka ndani ya chama chake.

Mgawanyiko huo uliosababishwa na kufichuliwa baruapepe zilizoonyesha alikuwa amependelewa na baadhi ya vigogo wa chama.

Siku ya kwanza ya mkutano huo, baadhi ya wafuasi wa waliokuwa wakimuunga mkono aliyekuwa mpinzani wake, Bernie Sanders walivuruga mkutano huo baada ya kubeba mabango ya kumuunga mkono Sanders, huku wakizomea wazungumzaji.

Hata hivyo, hotuba ya kusisimua iliyotolewa na mke wa Rais Obama, Michelle alisaidia kuleta utulivu.

Pia, Sanders aliwataka wafuasi wake kuzika tofauti zilizojitokeza na kuelekeza mapambano yao dhidi ya mgombea wa Republican.

Juzi usiku, Rais Barack Obama alitoa hotuba ya kusisimua akisema Wamarekani watakuwa salama zaidi iwapo watamchagua mgombea wa Democratic.

Alisema Clinton ndiye mtu wa uhakika na mwenye sifa zote za kumrithi Ikulu.

Kiongozi huyo alikuwa anawahutubia wajumbe wa Democratic na taifa kuhusu uwezo na sifa za mgombea wao, akisema anafika mwisho wa utawala wake bila ya kukamilisha aliyotaka kufanya.

Hivyo inabidi Wamarekani wamchague Hillary ambaye ana uwezo wa kuendeleza mipango yake.

Rais Obama alifafanua hoja moja baada ya nyingine kuhusu uwezo wa mgombea huyo aliyekuwa waziri wake wa Mambo ya Nchi za Nje na kwamba anawakilisha matabaka yote ya Wamarekani.

“Ninawaona Wamarekani wa kila chama, kila tabaka, kila imani wanaoamini kwamba tunakua na nguvu tukiwa pamoja. Weusi, walatino vijana, wazee, wanaume na wanawake wenye ulemavu wote ni wazalendo wa taifa hili kuu.”

Rais Obama aliwataka Wamarekani wamfanyie Clinton kile walichomfanyika miaka minane iliyopita kwa kumchagua kuwa Rais wa Marekani.

Kabla ya Obama kuzungumza, mgombea mwenza Time Kaine alikubali uteuzi wake na kujitambulisha kama mwanasiasa aliyeanza kuanzia daraja ya udiwani na kupanda kufikia gavana, seneta na sasa anatumaini kuwa makamu rais.

Awali, akizungumza kwenye mkutano huo uliomalizika jana, Makamu Rais Joe Biden pamoja na viongozi wengine wa chama hicho, aliwataka Wamarekani kutofanya makosa kwa kumchagua mtu ambaye anahubiri ubaguzi.

Alisema Clinton amedhihisha ndiye mwenye uwezo kurithi mikoba ya Obama .

“Marekani tusifanye makosa, Clinton ndiye chaguo sahihi kwa taifa letu.”

Clinton anategemea zaidi umahili wake wa kisiasa na uungwaji mkono kutoka Serikali iliyopo madarakani. Pia, kuibua kwa sera mpya hasa zile zinazolenga mabadiliko ya kiuchumi na kijamii.

Clinton anatarajiwa kuwashiwishi wasomi na wapigakura wengine nchini humo kwa kupinga matamshi ya chuki ya Trump dhidi yao.

Clinton amekuwa akikimezea mate kiti hicho tangu mumewe Bill Clinton alipokuwa rais wa nchi hiyo.

Miaka minane iliyopita Clinton alikaribia kuwa mwakilishi wa nafasi ya urais kwenye chama hicho nafasi ambayo ilikwenda kwa Obama ambaye alichaguliwa kuwa Rais wa Marekani.

Katika awamu ya kwanza ya utawala wake, Rais Obama alimteu kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wadhifa ambao alishikiliwa kwa kipindi cha miaka minne kabla ya kuomba kupumzika.

Clinton amekuwa akitazamwa kama mwanasiasa anayeleta chachu ya matumaini kwa vizazi vijavyo.