Obama awakumbusha wanasiasa mawazo ya Mandela

Muktasari:

Amewataka vijana duniani kote kufanyakazi kwa ajili ya kuhimiza haki za binadamu na jamii zinazotoa haki sawa.

Johannesburg, Afrika Kusini. Rais mstaafu wa Marekani, Barack Obama amewataka wanasiasa kuyafanyia kazi mawazo ya aliyekuwa kiongozi wa Afrika Kusini, hayati Nelson Mandela ambaye alipinga ubaguzi wa rangi.

Amasema hayo leo Jumanne akiwa kwenye maadhimisho ya miaka 100 ya kuzaliwa Mandela nchini humo akidai kwamba Mandela alikuwa akihamasisha demokrasia na uvumilivu.

Obama amesema wanasiasa wanatakiwa kuimarisha amani na upendo, wasiwe na siasa za chuki kwa kuwa hiyo ndiyo demokrasia inayotakiwa.

‘’Wanasiasa wale wenye nguvu wanajaribu kudhoofisha taasisi zote ... ambazo hutoa demokrasia” amesema.

Obama alikumbusha: "Tumekuwa katika nyakati za giza. Tumekuwa kwenye mabonde, Nasema kama watu wanaweza kujifunza chuki, wanaweza kufundishwa kupenda.”

Pia, amewataka vijana duniani kote kufanyakazi kwa ajili ya kuhimiza haki za binadamu na jamii zinazotoa haki sawa.

Amesema kwa sababu Mandela alikuwa anapambana kuleta maendeleo na haki sawa kwa wote, vijana hawatakiwi kurudi nyuma.