Ocean Road wasubiri bajeti kununua dawa

Muktasari:

Hata hivyo, tayari Serikali imetoa Sh1 bilioni kati ya Sh7 bilioni ilizotenga kwenye bajeti ya mwaka huu wa fedha kwa ajili ya ununuzi wa dawa za wagonjwa wanaotibiwa katika taasisi hiyo.

Dar es Salaam. Taasisi ya Saratani ya Ocean Road inaendelea kusubiri kukamilishiwa fungu la bajeti ililotengewa kwa ajili ya kununua dawa.

Hata hivyo, tayari Serikali imetoa Sh1 bilioni kati ya Sh7 bilioni ilizotenga kwenye bajeti ya mwaka huu wa fedha kwa ajili ya ununuzi wa dawa za wagonjwa wanaotibiwa katika taasisi hiyo.

Akizungumza wakati akipokea vifaa tiba na vya usafi vilivyotolewa na Taasisi ya Ukadiriaji Majenzi Tanzania (TIQS), Mkurugenzi mtendaji wa hospitali hiyo, Dk Julius Mwaisalage amesema upatikanaji wa fedha hizo utasaidia kumaliza tatizo la dawa linalotokana na ongezeko la wagonjwa wa saratani kila mwaka.

“Saratani ya shingo ya kizazi ipo juu na takwimu zinaonyesha kwa kila wanawake 100,000 nchini, kuna wagonjwa 58 wakati Marekani katika kila wanawake 100,000 wanane ndiyo wanakabiliwa na ugonjwa huo,”amesema.