Odinga abadili gia angani, ataka majadiliano

Muktasari:

Alisema timu yake iko tayari kwa mazungumzo "hata ingekuwa jana" muradi tu kikao kiwe ni namna gani uchaguzi huru na wa kuaminika unaweza kufanyika kulingana na amri ya Mahakama ya Juu na wala si juu ya kuunda serikali ya muungano.

Nairobi, Kenya. Kiongozi wa muungano wa upinzani (Nasa) Raila Odinga ‘amebadili gia angani’ na sasa anasema yuko tayari kwa mazumgumzo na Rais Uhuru Kenyatta, katika msingi uchaguzi uwe huru na wa haki na siyo kuunda serikali ya muungano.

Odinga ametoa msimamo huo wakati akitangaza kusitishwa kwa maandamano ya kuipinga Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Amesema badala yake, Nasa watafanya mikutano ya hadhara kuanzia Jumatano ili kuwaeleza wafuasi wao kwa nini uchaguzi mpya wa rais usifanyike Oktoba 26 kama ilivyopangwa na IEBC.

Alisema timu yake iko tayari kwa mazungumzo "hata ingekuwa jana" muradi tu kikao kiwe ni namna gani uchaguzi huru na wa kuaminika unaweza kufanyika kulingana na amri ya Mahakama ya Juu na wala si juu ya kuunda serikali ya muungano.

“Hisia ambazo zimejengeka ni kwamba mimi ndiye ninayetaka serikali ya nusu mkate,” alisema.

Kauli hiyo ilikuwa ya kurejea madai ya uongozi wa Jubile kwamba maandamano ya Nasa yalikuwa njama zilizolenga kuhakikisha kwamba Odinga na wenzake wanajumuishwa katika serikali ya muungano kama inavyokuwa baada ya vurugu zilizoibuka katika uchaguzi wa mwaka 2007/2008.

“Kamwe sijawahi kumwita Kenyatta na kutaka serikali ya muungano. Madai hayo, kwa hiyo ni ya upuuzi.”

“Ikiwa uchaguzi ni huru, haki na wa kuaminika, niko tayari wakati wowote. Nasa inataka kuunda serikali. Tunataka mkate kamili kwa sababu tulishinda. Tulishinda uchaguzi wa Agosti 8,”alisema akiwa katika Uwanja wa Ndege wa Wilson mjini Nairobi.