Friday, October 13, 2017

Marekeni yasikitika Odinga kususa uchaguzi

 

Nairobi, Kenya. Ofisa mmoja wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Marekani amesema kwamba nchi yake inaheshimu lakini imesikitishwa na hatua ya kiongozi wa upinzani (Nasa), Raila Odinga kujiondoa katika uchaguzi wa marudio uliopangwa Oktoba 26.

Akijibu swali aliloulizwa na gazeti la Nation, ofisa huyo alisema pia Odinga anakaribishwa kuitembelea Marekani.

Majibu hayo yanafuatia baadhi ya vyombo vya habari nchini kuripoti wiki hii kuwa Odinga alinyimwa viza ya kuingia Marekani. Madai hayo inaelezwa yalitolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Kidigitali katika Ikulu Dennis Itumbi.

Alipoulizwa ikiwa Odinga alizuiwa kuingia Marekani, ofisa huyo amesema, “Kwa uelewa wetu hakuna kizuizi kwa Raila Odinga kupanda ndege na kuruka hadi Marekani.”

Odinga yuko London, Uingereza ambako anatarajiwa kuhutubia leo katika Taasisi ya Uhusiano wa Kimataifa ya Royal.

Katika majibu yaliyotumwa Nation kwa baruapepe, ofisa huyo alisisitiza kwamba Marekani “haiungi mkono upande wowote wala mgombea yeyote” nchini Kenya.

“Sisi dhamira yetu ni kuunga mkono uchaguzi huru, wa haki na wa kuaminika kwa kuzingatia Katiba ya Kenya, sheria zilizopo sasa, na taasisi zake,” amesema ofisa huyo.

“Tunaheshimu haki za mgombea urais wa Nasa Raila Odinga na mgombea mwenza wake Stephen Kalonzo Musyoka ya kujiondoa kwenye uchaguzi wa Kenya uliopangwa Oktoba 26, lakini tunasikitishwa na uamuzi wake,” ameongeza ofisa huyo.

 

 

-->