Odinga amchelewesha Kenyatta kuapishwa

Muktasari:

Kwa uamuzi huo, Rais Kenyatta hataapishwa Agosti 29 kama ilivyotarajiwa bali itabidi asubiri hatima ya kesi hiyo ambayo inapaswa kusikilizwa katika muda usiozidi siku 14. Kwa hali hiyo ikiwa Mahakama ya Juu itatupa kesi hiyo, Kenyatta ataapishwa Septemba 12 lakini ikiwa ushahidi utaonyesha wizi, Wakenya watarudi kwenye uchaguzi.

Nairobi, Kenya. Hatimaye uongozi wa muungano wa upinzani wa Nasa umeamua kwenda Mahakama ya Juu kupinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu yaliyompa ushindi Rais Uhuru Kenyatta.

Kwa uamuzi huo, Rais Kenyatta hataapishwa Agosti 29 kama ilivyotarajiwa bali itabidi asubiri hatima ya kesi hiyo ambayo inapaswa kusikilizwa katika muda usiozidi siku 14. Kwa hali hiyo ikiwa Mahakama ya Juu itatupa kesi hiyo, Kenyatta ataapishwa Septemba 12 lakini ikiwa ushahidi utaonyesha wizi, Wakenya watarudi kwenye uchaguzi.

Msimamo wa Nasa kwenda kortini umekuja siku chache baada ya Rais Kenyatta kumtaka Odinga asitumie njia zinazoweza kusababisha machafuko bali kwenda mahakamani kupata haki yake. Pia umekuja baada ya Umoja wa Mataifa (UN) kukataa ombi la Odinga kuhakiki matokeo ya uchaguzi huo uliofanyika Agosti 8.

Msimamo wa Nasa

Akitoa msimamo huo jana, kiongozi mkuu na aliyekuwa mgombea urais wa Nasa, Raila Odinga alisema hatua hiyo, iliyofikiwa baada ya kushauriana na wadau mbalimbali pamoja na asasi za kiraia, itawawezesha kufichua namna Kenyatta alivyopata ushindi huo kwa kuvuruga kompyuta.

Raila aliwaambia wafuasi wake kwamba hawatakubali “uongozi uliotengenezwa kwa kompyuta.”

Awali muungano huo ulisema mwaka huu usingepeleka kesi kortini lakini baada ya vikao vingi, wameona ni heri kufanya hivyo “kufichua uovu uliotokea wakati wa uchaguzi mkuu.”

“Tumeamua kwenda kortini kufichua jinsi uongozi wa kompyuta ulivyofanikishwa,” alisema Odinga. “Hawa ni viongozi wa kompyuta. Kompyuta ndiyo iliwataga, kompyuta iliwaangua, na kompyuta iliwatotoa. Hawa ni vifaranga vya kompyuta.”

Kiongozi huyo amesisitiza msimamo wa Nasa kwamba uchaguzi haukuwa huru na wa haki kinyume na maoni ya waangalizi wa kimataifa.

Alisema mitambo ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilidukuliwa na matokeo yakavurugwa kumwezesha Kenyatta kuweka pengo kati yake na Odinga muda wote wa kutangazwa kwa matokeo.

Umoja wa Mataifa

Wiki iliyopita Odinga aliutaka Umoja wa Mataifa kuingilia kati kwa kuunda jopo la wataalamu ili wahakiki matokeo, lakini Katibu Mkuu wa UN, Antomio Guterres amekataa.

Odinga aliwasilisha ombi hilo katika mahojiano aliyofanya na gazeti la Financial Times la Uingereza akisema, “Tutaonyesha ulimwengu mchezo ulivyochezwa na kile tunachotaka ni Umoja wa Mataifa kuteua jopo la wataalamu ambalo litatusaidia kutathmini matokeo hayo.”

Katika mahojiano hayo, Odinga alisema IEBC ilikuwa chini ya shinikizo kali kutoka kwa maofisa wa serikali inayoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta. “Baada ya kuuawa kwa mtaalamu wa masuala ya Tehama katika tume hiyo Chris Msando, wafanyakazi wengine walikuwa na hofu. Kile kilichotokea kimeshinikizwa na serikali. Si kuhusu mimi na siyo kuhusu Raila Odinga mimi sitakuwa mgombea tena ila tunataka Wakenya wajue kilichofanyika, kile ambacho dunia nzima haielewi kinafanyika,” alieleza.

Aliongeza, “Hakuna haja ya watu kwenda kupanga milolongo mirefu ya kupiga kura kwa saa kadhaa au kufanya kampeni wakati kompyuta moja katika tume ya IEBC inatumiwa kuchakachua matokeo hayo”.

Katibu Mkuu wa UN, Antonio Guterres alikataa ombi hilo na badala yake alishauri viongozi wa kisiasa ambao hawajaridhika na matokeo hayo kwenda mahakamani ambayo ni “taasisi muhimu yenye mamlaka hayo kikatiba.”

Kadhalika, Msemaji wa UN, Farhan Haq alirudia msimamo huo wa Guterres wa kuwashauri Odinga na wenzake kutumia njia hiyo ya kikatiba na kwamba Umoja wa Mataifa utafuatilia.