Ofisa TRA, polisi wapandishwa kizimbani

Muktasari:

Watuhumiwa hao wanadaiwa kutenda kosa Aprili Mosi katika kizuizi cha magari kilichopo Kijiji cha Kirumi wilayani Butiama

Musoma. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Mara, imewafikisha mahakamani polisi wawili na ofisa mmoja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa ya Sh10 milioni.

Watuhumiwa hao walifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mara juzi, mbele ya hakimu Jacob Ndila na kusomewa makosa matatu.

Mwendesha mashtaka wa Takukuru, William Fussi aliwataja washtakiwa hao kuwa ni ofisa wa TRA, Proches Kavishe (27), mkaguzi msaidizi wa jeshi la polisi Idrissa Majamba (37) na Zakayo Mngulu polisi.

Hata hivyo, Mngulu hakufikishwa mahakamani baada ya kudaiwa kutoroka katika kituo chake cha kazi mjini Musoma. Fussi alieleza kuwa watuhumiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo Aprili Mosi mwaka huu katika kizuizi cha magari kilichopo Kijiji cha Kirumi wilayani Butiama saa tatu usiku.

Alifafanua kuwa siku hiyo watuhumiwa waliomba Sh40 milioni kwa wafanyabiashara wawili ili waruhusiwe kupita na malori yaliyokuwa yamebeba bidhaa mbalimbali za biashara.

Alidai kuwa ingawa wafanyabiashara hao walifuata taratibu zote za kuingiza bidhaa zao nchini na kulipia vibali katika kituo cha TRA kilichopo Sirari wilayani Tarime, maofisa hao waliwalazimisha kutoa fedha hizo kama kishawishi ili wawaruhusu kuendelea na safari zao.

Fussi alidai kuwa kutokana na hali hiyo wafanyabiashara hao waliomba kupunguziwa kiwango cha fedha na hatimaye walikubaliana kutoa Sh10 milioni ili waachiwe.

“Wafanyabiashara hao walitoa fedha ambazo zilitumwa kwa njia ya mtandao wa simu kupitia kwa wakala mmoja wa huduma za kifedha, kisha walitoa taarifa Takukuru ambao walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa wote watatu,” alidai mwendesha mashtaka.

Watuhumiwa hao wawili wako nje kwa dhamana na kesi yao itatajwa tena Julai 24 mwaka huu.