Ofisa elimu aagiza mwalimu atupwe rumande kwa madai ya kuoa mwanafunzi wake

Muktasari:

Siperato alitoa agizo hilo jana Agosti 20 na kumtaka Mwalimu Ikila afike ofisini kwake leo akiwa ameambatana na mwanafunzi huyo


Buchosa. Ofisa Elimu wa Sekondari ya halmashauri ya Buchosa Wilayani Sengerema, Mwanza, Benjamin Siperato ameagiza kuswekwa mahabusu Mwalimu Michael Ikila wa shule ya Sekondari Nyakasungwa.

Siperato ametoa agizo hilo baada ya Mwalimu Ikila kukaidi agizo lake la kuambatana na mwanafunzi anayedaiwa kumuoa.

Badala yake Mwalimu Ikila alikwenda peke yake kwenye ofisi ya Ofisa Elimu huyo leo asubuhi.

Siperato alitoa agizo hilo jana Agosti 20 na kumtaka Mwalimu Ikila afike ofisini kwake leo akiwa ameambatana na mwanafunzi huyo .

Mwanafunzi huyo (jina linahifadhiwa) anayepaswa kuwa kidato cha tano mwaka huu anadaiwa kuolewa na mwalimu wake (Michael Ikila) tangu mwaka jana alipohitimu kidato cha nne.

"Baada ya kupokea taarifa za Mwalimu kumuoa mwanafunzi wake nikaagiza amlete mwanafunzi huyo ofisini kwangu leo Agosti 21 lakini hajatimiza agizo langu. Nimeagiza awekwe mahabusu," amesema Siperato.

Ofisa elimu huyo amesema ofisi yake inaendelea kufuatilia kwa makini suala hilo huku akionya kuwa hatua zaidi zitachukuliwa dhidi ya mwalimu yeyote anayekiuka maadili.

"Pamoja na kuchukua hatua dhidi ya mwalimu, ofisi yangu pia inafanya kila linalowezekana kumsaidia mwanafunzi aliyeathiriwa," amesema Siperato

Mwalimu Ikila anatuhumiwa kumuoa mwanafunzi wake, mnamo mwaka jana.

Mkuu wa shule ya Sekondari Nyakasungwa Safari Mashimba alipoulizwa juu ya mwalimu kusekwa rumande amesema hana taarifa hiyo anachofahamu alimuaga kuwa ameitwa wilayani.