Ofisa mifugo asimamishwa kazi Kiteto

Muktasari:

Fedha hizo ni kwa ajili ya gharama ya upigaji chapa mifugo wilayani humo, ambapo lengo ni kufikia mifugo 363,128 kati 247,425 iliyopo wilayani humo.


Kiteto. Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto, Mkoani Manyara, Tamim Kambona amemsimamisha kazi Ofisa mifugo wa wilaya hiyo William Msuya kwa tuhuma za ubadhirifu wa sh60 milioni za chapa ya mifugo.

Fedha hizo ni kwa ajili ya gharama ya upigaji chapa mifugo wilayani humo, ambapo lengo ni kufikia mifugo 363,128 kati 247,425 iliyopo wilayani humo.

Kambona amesema  wakati wa zoezi hilo baadhi ya wafugaji walipewa risiti na wengine kunyimwa kwa makusudi na ulipofanyika ukaguzi walibaini upotevu wa fedha hizo.

Amesema  pamoja na kutakiwa kuwasilisha fedha hizo na kikao cha fedha na mipango, Msuya alikaidi na hata kutofika kazini huku akimtuma msaidizi wake kwenye vikao vya kazi.

“Nimempa siku 14 arejeshe fedha hizo mara moja tena aingize benki na kuniletea risiti hata kwenye vikao anatuma msaidizi, kwa sasa anakuja kazini kwa muda anaotaka, kama hatorejesha mimi nitamfikisha mahakamani,” amesema  Kambona.

Amesema  hatosita kumchukulia hatua mtumishi yoyote atakayeonekana kuihujumu halmashauri na kutoa onyo kwa watumishi wa idara hiyo ya mifugo kuwa bado kuna watumishi ambao wameshiriki katika wizi huo kuwa nao wajiandae.

Diwani wa kata ya Namelock, Michael Lepunyati amesema  amelazimika kuwa mfano wa kupiga zoezi hilo ili jamii ya kiufugaji  waweze kuiga kwani awali walikataa kwa madai kuwa chapa hiyo inafanya mifugo kutozaa.

“Tumekubaliana wafugaji wote baada ya kutolewa elimu tulianza na kundi la viongozi, tena kwa kuchangia fedha ambazo ni utaratibu wa zoezi hilo ili wafugaji waone hakuna madhara,” amesema  Lepunyati.

Hata hivyo, Msuya alipopigiwa simu ili azungumzie juu ya hilo hakupokea na pia alipotumiwa ujumbe mfupi kwa ajili ya kutoa ufafanuzi hakujibu.